NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 01 - 05

NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 1:

Ilikuwa kwenye mida ya saa mbili usiku wakati tumekaaa kwaajili ya chakula cha usiku.
Wakati nakula simu yangu ikaita kuangalia mpigaji ni mpenzi wangu Sam ila nikashindwa kunyanyuka kwenda kupokea kwani mama alikuwa ananiangalia sana ikabidi nibonyeze kitufye cha kimya (silence).
Mama kumbe alisikia wakati inaita akauliza,
"Nani anakupigia wakati wa kula?"
"Hakuna mtu mama, ni alarm tu"
"Unadhani sijasikia wakati inaita? Umeanza uongo eeh!!"
"Hapana mama ni Sam"
"Nilijua tu, anakupigia wakati wa kula amekununulia hiyo simu? Anaijua bei yake?"
Ikabidi nikae kimya, mama yangu alikuwa anamchukia sana Sam. Hakupenda kabisa mahusiano ya mimi na Sam ingawa tulipendana sana.

Tulipomaliza kula tulikuwa tumekaa sebleni, nikatamani kuinuka kwenda chumbani nikazungumze kidogo na Sam na kumwambia kuwa muda aliokuwa anapiga nilikuwa nakula.
Nikawa nainuka, mama akaanza kuongea kabla hata sijaanza kutembea.
"Unaenda wapi Sabrina?"
"Naenda chumbani mara moja mama"
"Kuongea na simu eeh!! Amekupa nini huyo Sam jamani? Yani unashindwa kukaa hapa kuzungumza na mama yako na chakula kitulie, wewe macho juu juu kukimbilia ndani kuongea na Sam. Amekuwa mzazi wako huyo? Sipendi hiyo tabia, haya kaa tuzungumze ya maana hapa"
Ikabidi nikae ila mawazo yangu yote yalikuwa ni kwa Sam tu hata maneno ambayo mama alizungumza sikumuelewa hata kidogo, nikaona anapiga kelele tu.
Nadhani pale aliyekuwa anamsikiliza ni dada yangu Penina tu maana ndio waliokuwa wakijibishana.
Mama akaniomba simu yangu na kupigia ndugu zake, akaongea wee hadi muda wa maongezi ulipokata ndio akanirudishia. Nikabakiwa na ujumbe mfupi tu bila ya muda wa maongezi.

Mama aliponyanyuka nami nikanyanyuka kuelekea chumbani, kisha nikamtumia ujumbe mfupi Sam kuwa anipigia. Naye hakusita kunipigia ila alinipa lawama mwanzo mwisho.
"Sabrina una dharau sana, yani simu yangu hupokei. Nangoja kidogo kupiga namba inatumika yani kuna watu unawaona wanathamani sana kushinda mimi. Poa tu Sabrina"
"Jamani Sam mpenzi wangu, tafadhari nisamehe"
"Umefanya makusudi wewe, poa tu mi nalala saivi"
Halafu akakata simu, nikajisikia vibaya sana ikabidi nimtumie ujumbe wa kumuomba msamaha ila Sam hakupiga wala kujibu ujumbe wangu.
Sikuweza kumwambia Sam kama mama yangu anamchukia kwani nilijua wazi kuwa akijua tu lazima atajisikha vibaya ukizingatia kwao mama yake ananipenda sana mimi.

Asubuhi na mapema nikapata ujumbe toka kwa Sam.
"Yani wewe Sabrina una dharau sana, sijui kwavile umejua nakupenda sana. Yani umeshindwa hata kunipigia simu upooze mawazo yangu umekazana na ujumbe tu!! Najua muda wote wa maongezi umemaliza kwa watu wako ila poa tu. Mimi nitaendelea kukupenda Sabrina"
Nikaamua kuamka na kwenda kununua vocha ili nipate kuzungumza na Sam.
Ila maduka yalikuwa bado hayajafunguliwa, nikaamua kuanza kufanya kazi mbalimbali za pale nyumbani ili niwahi kumaliza na niweze kwenda kwa Sam kwani nililuwa nimemkumbuka na pia nilitaka nikamweleweshe ya jana.
Baada ya kazi nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea rafiki yangu Suzy, mama hakuwa na pingamizi akaniruhusu niende nami nikaenda moja kwa moja kwa Sam ila sikumkuta na mlango wake ulikuwa na kufuri.
Ikabidi niende duka la karibu kununua vocha kisha nikampigia ila hakupokea nikajua tu kisirani kimempanda.
Nikaamua kuondoka na kwenda kweli kwa kina Suzy ili badae nipate kurudi tena kumuangalia.

Nilikaa sana kwa kina Suzy ila sikumueleza Suzy jambo lolote lile kuhusu Sam, badae nikaaga na kwenda tena kwa Sam nikawa namngoja kuwa pengine ameenda kazini ila ilikuwa ni mwisho wa wiki ndiomana nilijiamini na kwenda.
Nilimngoja sana Sam bila ya kutokea, nilikata tamaa na moyo kuniuma sana kuwa kwanini Sam amenifanyia vile kwa kosa dogo kiasi kile.
Nikajaribu kuwauliza na majirani ambao walisema kuwa Sam ameondoka asubuhi sana, nikajiuliza kuwa labda ameenda kwao ila kwanini asipokee simu? Nikaona kuwa Sam ananifanyia kusudi, hisia mbaya zikanitawala kuwa Sam atakuwa kwa mwanamke mwingine tu hapo roho ikaniuma sana.
Muda ulizidi kwenda, ikabidi nirudi nyumbani.

Nilifika nyumbani kwenye mida ya saa tatu usiku, nikamkuta mama na dada wakifanya maongezi ya hapa na pale.
Nikawasalimia na kwenda kuoga kisha kula chakula.
Dada akaanza kuzungumza,
"Halafu wewe Sabrina, kupenda kwako huko kutembea usiku usiku ipo siku utakumbana na majini huko njiani"
Nikashtuka sana na kumuuliza dada,
"Majini? Una maana gani dada?"
"Usiku ni mida ya majini, yakikukumba huko usituletee balaa hapa"
"Kwani majini yakoje?"
"Ukikutana nayo lazima nywele zisisimke, halafu ni marefu sana mara nyingine huwezi ona mwisho wa urefu wao"
"Mbona unanitisha dada?"
"Sikutishi ila huo ndio ukweli, unatakiwa kuwa makini sana. Majini hayana masikhara, likikuvaa ndio limekuvaa utakula nalo, kulala nalo na kuamka nalo bila ya kutarajia"
Nikaanza kuingiwa na uoga, mama nae akaanza kuchangia hoja zake.
"Unakumbuka kule makaburini wakati wanamzika yule dada mwenye mashetani kilichotokea?"
Dada akajibu,
"Ndio nakumbuka mama, yani majini hayataki mchezo"
Ikabidi niulize tena,
"Kwani majini yanafanana na kitu gani"
"Majini yanatisha mdogo wangu usiombe ukutane nayo njiani unaweza usilale siku mbili unaweweseka tu."
"Inamaana yanaweza kutokea wakati mtu amelala?"
"Ndio, unaweza ukashangaa umelala na jini pembeni yako"
Niliogopa sana na kuwaza kwanini nimesikiliza habari za majini usiku.
Mama akaongezea kitu kingine ambacho kilifanya niende chumbani kumtafuta Sam.
"Ila leo umenifurahisha kitu kimoja, kwenda kweli kwa Suzy maana huyo Sam wako amekuwa hapa siku nzima kukungoja"
Nikagundua kuwa, wakati mimi namngoja Sam kule kwake kumbe na yeye alikuwa kwetu kuningoja ila kwanini hakutaka kupokea simu yangu.

Nikaenda zangu chumbani kwa lengo la kumpigia tena Sam simu.
Ila nikasita kwani nikaona Sam nae ananifanyia kusudi, kama kweli alikuwa kwetu kuningoja kitu gani kimemfanya asipokee simu yangu. Mara dada akaniita na kufanya yale mawazo yangu juu ya Sam yakatike.
"Vipi Sabrina ndio unataka kulala muda huu?"
"Ndio dada, nataka kulala"
"Njoo mara moja, kuna kitu nataka unisaidie huku chumbani kwangu"
Nikatoka na kufatana na dada hadi chumbani kwake.
"Kuna kitu kinanichanganya hapa kwenye computer yangu, naomba uniondolee hii picha"
Mimi nikaitazama ile picha, ilikuwa ni ya mwanaume mzuri sana. Nikamuuliza dada kuwa kwanini anataka kuifuta,
"Kwanini uifute dada? Mbona picha yenyewe ni nzuri?"
"Hata sielewi nimeidownload vipi hiyo picha hadi imekaa hapo, nitolee bhana mipicha mingine inaweza kuwa ya majini"
"Mbona unapenda sana story za majini dada?"
"Yapo na ndiomana nayaongelea, usishangae siku ukitokewa na jini"
"Basi yaishe, mi sitaki tena hizo habari nisije kushindwa kulala bure"
Nikafanya ninachojua kuifuta ile picha kisha nikamuaga dada usiku mwema na kuondoka.

Nikarudi chumbani na kuendelea kuwaza kuhusu Sam wangu. Wakati nikiwaza juu ya Sam, wazo la majini likanijia tena kichwani nikajikuta naanza kuogopa chumbani halafu ile picha ambayo dada aliniomba kuwa nimsaidie kufuta ikawa inatembea kichwani mwangu.
Niliona chumba kimekuwa kikubwa sana, nilipokaa kitandani nilihisi kama vile kuna mtu pembeni yangu nikaanza kuogopa zaidi huku nikijilaumu kuwa kwanini nimesikiliza stori za kutisha muda wa kulala.
Nikachukua tena simu na kuamua kumpigia Sam ili kujiliwaza kidogo ila kabla sijapiga nikapitiwa na usingizi.

Mwanaume mzuri sana na mtanashati alikuwa mbele yangu, asili yake kama mwarabu hivi au muhindi.
Alikuwa anatabasamu na kusogea taratibu kuja mahali ambako mimi nipo.
Nilikuwa namwangalia kwa jicho la mshangao tu.
Alipofika karibu yangu, akanivuta mkono kisha akatoa kitu cha ajabu kilichofanya nishtuke.

NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 2:

Akanivuta mkono kisha akatoa kitu cha ajabu kilichofanya nishtuke.
Nikajikuta jasho jingi likinitoka pale kitandani, nikawa najiuliza kuwa ni ndoto ya aina gani na inamaanisha kitu gani? Je huyo mwanaume mzuri sana kushinda Sam wangu ni nani?
Hapo ndio nikakumbuka kuwa natakiwa kumpigia Sam simu.

Nikaangalia simu yangu na kuichukua kisha nikaibonyeza, nikakuta simu ambazo hazijapokelewa kumi (10 missed call), kuangalia zote ni kutoka kwa Sam na ujumbe mfupi tano (5 messages).
Kila ujumbe ulikuwa ni wa lawama tu kutoka kwa Sam, nikaona haya majanga sasa.
Nikabonyeza simu na kuanza kupiga nikasikia,
"Salio lako halitoshi kupiga simu, tafadhari ongeza........."
Nikaishusha ile simu na kuikata, kuangalia kweli nimebakiwa na sifuri nikaanza kujiuliza kuwa nimeitumiaje ndipo nikakumbuka kuwa nilinunua salio na kusahau kujiunga na huduma za bure na wakati narudi nyumbani nilimpigia Suzy na kuongea nae sana tu nikijua nimejiunga kumbe sikujiunga, vocha yangu yote ya elfu mbili imekwenda bure bure bila hata ya faida sikujua cha kufanya kwa wakati huo.
Nikatamani niende chumbani kwa mama nikachukue simu yake na kuhamishia salio lake kwangu kama ana salio.
Nikainuka pale kitandani na kusogelea mlango kisha nikafungua, wazo la stori za majini likanijia tena kichwani na kujikuta nikiubamiza ule mlango kwa kuufunga na kurudi tena kitandani, nikajiuliza kuwa kwanini ile stori ya majini imenikaa sana kichwani mwangu? Nikaanza tena kufikiria ile ndoto kuwa ilikuwa na maana gani kwangu.
Sikuweza kulala tena kwa uoga na pia bado nilikuwa na mawazo juu ya Sam.

Asubuhi yake, mimi ndio nilikuwa wa kwanza tena kuamka, nikafanya usafi na kazi za hapa na pale nyumbani huku nikingoja pakuche vizuri nikanunue vocha ya kuweza kumpigia Sam.
Nilipomaliza usafi nilirudi tena chumbani, nikajilaza kitandani na usingizi ukanichukua hapohapo.

Yule mkaka mtanashati akaanza kunionyesha mali zake, zilikuwa nyingi sana. Kumbe yule mkaka alikuwa tajiri, akanionyesha magari ya aina nne halafu akaniambia kuwa nichague moja liwe langu naye atanipa lotelote, nikawa natabasamu kwani magari yalikuwa mazuri sana na ndoto zangu siku zote ni kuwa na gari ila gafla nikakumbuka kuwa nina Sam wangu ambaye hawezi kunipa vyote vile ila anaweza kunipa mapenzi ya dhati, nikajikuta nikishtuka na kupiga kelele.
"Saaaaaaaaaammmmmm....."
Mama akaja chumbani na kusema.
"Wee Sabrina wewe, usiniletee uchuro nyumbani kwangu. Yani wewe kuamka tu na kumtaja Sam! Amekuwa Mungu huyo Sam?"
"Hapana mama, ila nimeota vibaya"
Jasho nalo lilikuwa lanitoka.
"Umeota vibaya kivipi? Umeota Sam anachinjwa au?"
"Hapana mama."
"Haya inuka hapo, kuna mboga ya kukata kata huku"
Nikainuka tena pale kitandani na kumfata mama jikoni, kisha kukiendea kisu na kukata kata ile mboga.
Mawazo yalikuwa ni juu ya ile ndoto na yale magari, kisha nikakumbuka tena kuwa nilitakiwa kununua vocha na kumpigia Sam.
Nilikata mboga haraka haraka na kuibandika jikoni kisha nikajitanda vizuri ili niende dukani kwanza.
Kabla sijatoka mama akauliza,
"Unaenda wapi Sabrina?"
"Naenda dukani mama."
"Kufanya nini?"
"Kununua vocha mama"
"Ili umpigie Sam eeh!! Sijui huyo mwanaume amekupa nini mwanangu unakuwa kama chizi"
Sikutaka kumsikiliza zaidi kwani nilijua kuwa lazima atanizuia tu.

Nilinunua vocha na kurudi nyumbani. Nikamkuta mama sebleni,
"Huna adabu mwanangu Sabrina, yani umeona vocha ya maana kuliko maneno yangu? Vocha ambayo pesa nakupa mimi!!"
Nilibaki kumuangalia tu mama na maneno yake kwani nilijua yote sababu hataki niwasiliane na Sam.
"Haya lete hiyo vocha haraka"
Nilimpa ile vocha mama kwa shingo upande kwani moyo uliniuma sana, nikatamani hata kuwa na maisha ya kwangu. Nikatamani kutoa machozi mbele yake ila nikajizuia kwa kufumba macho ili mama asinione mzembe, ingawa na kujizuia kule bado machozi yalipenya na kudondoka mashavuni mwangu.
"Kaone kalivyo kajinga, eti kanamlilia mwanaume. Hebu niondolee uchizi wako mbele yangu haraka"
Nikaondoka na kukimbilia chumbani, huko nililia nitakavyo katika kupooza uchungu wangu.
Nilipotazama tena simu nikaona ujumbe wa Sam tena wa kutosha, sikuweza kujibu hata jumbe moja kwa kukosa vocha. Nikajikuta nikiulaumu mtandao ninaotumia pia kwa kushindwa kutuma tafadhari nipigie.
Nilizidi kutokwa na machozi tu mule ndani.

Wakati nalia nikasikia mtu akigonga mlango wa chumba changu, nikashtuka na kujiuliza ni nani maana dada na mama hawanaga hodi, huwa wanaingia tu chumbani.
Nikamuitikia kuwa aingie ndani, huku nikimaliza kujikausha machozi yangu. Kumbe alikuwa ni rafiki yangu mpenzi Lucy, nilifurahi kumuona nikainuka pale kitandani na kumkumbatia, nikamkaribisha vizuri sana.
Kumbe Lucy naye alishangazwa na hali aliyonikuta nayo,
"Nimekungoja sana hapo sebleni kwenu ndipo mama yako aliposema nikufate chumbani eti umechukia sababu ya mwanaume. Mmh! Mwanaume gani tena huyo Sabrina?"
Nikamueleza kwa kifupi kuhusu Sam kwani Lucy alikuwa hajui chochote kuhusu Sam.
"Inamaana kushindwa kuwasiliana nae ndio kunakuliza jamani shoga yangu? Chukua basi simu yangu uwasiliane nae maana ina muda wa kutosha"
Nikachukua simu ya Lucy na kumpigia simu ambapo alishangaa kuona namba ngeni.
"Mbona namba mpya hii, ni ya nani?"
"Ni ya rafiki yangu mmoja anaitwa Lucy ila wewe humjui, ipo siku utamjua"
Wakati nazungumza na Sam, Lucy nae akaniomba simu ili amsalimie shemeji yake huyo, nami nikamkabidhi.
Baada ya salamu tukazungumza na Sam kisha tukapatana tena na kusameheana kwa yote yaliyopita halafu Sam akanitumia vocha ili niache kumpigia kwa namba mpya.

Kilichobaki ilikuwa ni stori na vicheko baina yangu na Lucy.
"Mmh shemeji ana sauti ya kuvutia huyo, yaonyesha atakuwa handsome sana"
"Mmh Lucy ushaanza maneno yako, hukui wewe?"
"Kwani nikimsifia shem wangu kuna ubaya Sabrina?"
"Hakuna ubaya"
"Ila ningependa kumfahamu zaidi, natumaini ipo siku utanikutanisha nae"
Niliongea mengi sana na Lucy ila alikazana sana kumsifia Sam hadi akawa ananipa mashaka ila sikuyatilia maanani sana.
Lucy alipoaga, nilimsindikiza akaondoka.

Jioni ilipoingia kama kawaida ya siku hizi za karibuni, wakaanza tena stori zao za majini na aliyeanzisha alikuwa ni dada yangu Penina.
"Jamani Posta kuna mambo, yani mtu niliyepishana nae ni dhahiri kabisa alikuwa jini maana nywele zote zilinisimama"
Mama nae akadakia,
"Ulikuwa hujui mwanangu? Yani Posta na Kariakoo hakuwezi kukosa majini kule, unadhani unaopishana nao huko wote ni watu basi! Nusu yao ni majini"
Nikaanza kuogopa tena kwa yale maneno na hata sikujua kwanini mimi yaliniogopesha wakati wao walioyaongea hawakuogopa.
"Hivi jamani, kwanini ikifika usiku ndio mnaanza hizo stori za majini? Hakuna stori zingine?"
Dada akaanza kunicheka kuwa kwanini naogopa wakati ni kitu cha kawaida tu.
"Sasa wewe Sabrina unaogopa nini? Unadhani yatakutokea?"
"Naogopa tu jamani"
Mara mama akanitisha,
"Haya, huyo nyuma yako"
Nilipiga kelele na kurukaruka, huku wote wakiwa wananicheka.
"Hutakiwi kuogopa mwanangu, haya ni mambo ya kawaida na wengi yanawapata ndiomana tunayaongelea. Na ukitaka kutokuogopa kitu basi wewe kizoee"
"Ndio kuzoea majini mama?"
"Hapana si kuzoea majini, ila stori hizi uzione kama kawaida na hautapata shida tena"
Wakaendelea kusimuliana mambo ya watu wanaofufuka na majini.
Ikabidi nimuulize dada kuhusu ile picha aliyoniomba niifute jana yake.
"Dada, nakumbuka uliniambia kuwa majini ni mabaya na sura zao zina tisha. Mbona yule mkaka mzuri ulisema tufute picha yake kuwa huenda akawa jini?"
"Nilikuwa najisemea tu ila hata hivyo majini yanamtindo wa kubadilika kama kinyonga"
Mama akaingilia mazungumzo yetu.
"Kumbe na wewe Sabrina unawajua wakaka wazuri? Mbona ukampenda Sam basi?"
Dada akanisaidia kujibu,
"Ila Sam sio mbaya jamani mama, humpendi tu sababu ya kipato ila usisingizie uzuri"
Nikawaacha na kwenda chumbani kwangu. Nikaenda kuoga kisha kujiandaa kulala.

Usiku wa leo ulikuwa na uoga kiasi kwangu na furaha pia kwani vocha nilikuwa nayo na Sam nilishapatana naye.
Nilipokuwa tu kitandani nikampigia Sam simu ili kupotezea yale mawazo ya stori ambazo mama na dada walikuwa wakisimuliana.
Niliongea sana na Sam kwenye simu hadi saa saba usiku kisha nikapitiwa na usingizi huku simu ikiwa sikioni.

Nilikuwa ufukweni (beach) na Sam tukifurahia upepo na kuchezea maji. Sam alivaa nguo nyeupe na mimi nilivaa gauni la pinki, tulifanya mambo mengi sana ambayo wapendanao huwa wanafanya.
Tukaanza mchezo wa kufunikana macho kwa nyuma na wakati huo Sam alikuwa nyuma yangu na mikono yake imepita juu ya mabega yangu kisha viganja vyake vilifunika macho yangu, akaanza kunitembeza na kunipeleka nisipopajua.
Kufika mbele akaniuliza,
"Nikufumbue macho nisikufumbue?"
Nami nikamjibu kwa sauti ya taratibu tena ile ya kudeka,
"Nifumbue bwana"
Basi Sam akaachia vile viganja vya mikono yake nami nikapata kuona kilichopo mbele yangu, nikamuona yule mkaka wa kwenye ndoto akiwa mbele yangu na alivaa nguo nyeupe tupu kuanzia kiatu, suruali hadi shati.
Nikajikuta nikitetemeka ila yeye alikuwa akitabasamu, nikaangalia nyuma yangu kama yupo Sam ila hakuwepo na sikujua ameelekea wapi, nikaanza kukimbia huku yule mkaka akinifata nyuma alipokaribia kunishika nikashtuka kumbe nilikuwa naota.
Jasho jingi lilinitoka, kutazama nje kulikuwa kumekucha kabisa yani kama sio saa mbili basi ni saa tatu.
Kabla sijafanya chochote, simu yangu ikawa inaita kuangalia ni Sam anapiga basi nikaipokea, baada ya salamu nikamsikia.
"Uwahi kujiandaa mpenzi ili badae twende beach, sawa Sabrina. Halafu uvae lile gauni lako la pinki"
Niliendelea kuweka ile simu sikioni bila ya kujua cha kujibu.

NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 3:

Niliendelea kuweka ile simu sikioni bila ya kujua cha kujibu.
Upande wa pili nao ulishangazwa na kimya changu na kuuliza,
"Vipi mpenzi mbona kimya? Hujanielewa au?"
Nikajikaza kumjibu kwa sauti ya upole,
"Ndio sijakuelewa"
"Nimekwambia kuwa uwahi kujiandaa kwaajili ya ile safari yetu ya beach na uvae gauni lako lile la pinki. Bado hujaelewa?"
Nikaishusha ile simu taratibu, sauti ya mama ikanishtua ambapo alifungua mlango bila ya hodi kama kawaida yake na kuanza kuongea.
"Yani mtoto wa kike ndio unaamka saa nne hii, halafu kitu cha kwanza ni kukumbuka hilo pepo lako chafu la simu"
Nikajikuta nikiiachia ile simu kwani nilishangaa kuwa muda ule ni saa nne sema kwa bahati ilikuwa ni kwenye kitanda ndio ikaangukia hapo.
"Mbona umetoa macho tu hata hunijibu wakati simu umeongea nayo?"
"Jamani mama hata salamu? Shikamoo."
"Haina umuhimu saa nne hii, kazi zote umeniachia mamako kama vile sikuzaa jamani!! Haya inuka hapo kitandani uje huku"
Halafu akatoka, nikamshangaa mama kuongea vile wakati si kawaida yangu kulala sana mpaka kupitiliza kiasi kile. Na hata kama nikilala vile basi ni kwamba kuna muda niliamka na kufanya kazi kisha kurudi tena kulala ila siku hiyo nilipitiliza hadi kujishtukia.

Nikajitoa chumbani na kwenda jikoni kumuomba mama msamaha kwa kuchelewa kuamka.
"Unaona kama nakukera mwanangu ila mimi nakufundisha hata utakapoolewa uwahi kuamka, hakuna mwanaume anayependa kuishi na mke mvivu. Yani hadi saa nne mwanamke hajaamka, hajafanya usafi wala kuandaa chai. Nakwambia kwa mtindo huo mwanaume lazima akuache, mwanamke mwingine anamuachia kazi zote msichana wa kazi hadi kazi za mumewe, mwisho wa siku mume anachukua msichana wa kazi badili ya mke. Nakufundisha kazi mwanangu, sijui kama unanielewa!"
"Nakuelewa vizuri sana mama yangu"
"Itabidi nikupe darasa kabisa na kama ukilifata basi kuachika usahau kabisa na kama huyo mume akikuacha basi atakuwa na hila ya kwapa kunuka bila kidonda"
Kwakweli mama yangu alikuwa ni muongeaji sana hadi kipindi wakati baba yupo alikuwa anamuita mama kasuku na tulikuwa tunacheka sana.
"Sasa mama utanipa lini hilo darasa? Nipe leo basi"
"Kwani unataka kuolewa? Hebu nitolee uchuro wako mie nionekane nina uchu sana wa mahari yako."
"Kwani mama mi sifai kuolewa?"
"Nikuoze kwa kale kajamaa kale!! Katanipa nini mimi? Hebu nenda kwanza kaoge huko"
Nikajiinukia kwa unyonge na kwenda kuoga.

Niliporudi chumbani nilikuta simu yangu inaita na mpigaji alikuwa ni Sam, nikaipokea ile simu.
"Mbona unadharau hivyo Sabrina? Kweli wewe wa kutokuijibu simu yangu jamani!!"
"Nisamehe mpenzi wangu"
"Ndio unachoweza kusema hicho, unakumbuka tulichopanga usiku wakati tunaongea kwenye simu?"
"Nimesahau Sam"
"Nakata simu halafu nakupa dakika kumi uwe umekumbuka, nitakupigia tena kunipa jibu"
Halafu Sam akaikata ile simu, nikajikuta nikianza kurudisha mawazo ya nyuma kichwani mwangu.
Nikakumbuka kuwa niliongea na Sam hadi usiku sana ila sikukumbuka tumeongelea kitu gani, mara kumbu kumbu za ndoto zikanijia hadi pale ambapo Sam aliponipigia simu ni hapo nilipojituliza akili na kujiuliza kuwa kuna mahusiano gani ya yule mwanaume wa kwenye ndoto zangu na Sam? Na kwanini Sam aniambie nivae gauni la pinki ambalo limetokea kwenye ndoto zangu?
Wakati natafakari hayo simu yangu ikaanza kuita, nilipoona kuwa ni Sam nikajua tu kuwa anayataka majibu yake. Nikapokea ile simu,
"Haya niambie ulichokumbuka"
"Kwakweli tuliyoyaongea usiku sikumbuki kabisa ila ninachokumbuka ni tulichoongea asubuhi"
"Ok, hiyo asubuhi nilisemaje?"
"Ulisema kuwa niwahi kujiandaa ili twende beach na nivae gauni langu la pinki"
"Sawa sawa, kumbe kumbe kumbukumbu unayo. Sasa kwanini hukumbuki vya usiku? Na je ushajiandaa kwa safari?"
"Bado sijajiandaa"
"Kwanini unanifanyia hivyo Sabrina jamani? Unajua mambo mangapi nimeacha kwaajili yako? Mbona unadharau kiasi hicho?"
"Hapana Sam"
"Kwanini Hapana?"
"Kwanini uchague gauni la pinki? Na mbona umenishtukiza na hiyo safari wakati siku zote huwa nakwambia kwamba uniambie mapema? Unanionea tu Sam na yote sababu unapenda ubabe"
"Naomba uelewe Sabrina, kwanza kabisa hii safari si ya kushtukiza. Jana usiku tumejadili wote kwenye simu kuwa leo twende beach, halafu kuhusu swala la nguo ulilianzisha mwenyewe jana na ukasema kuwa mimi nivae shati nyeupe na ukaniuliza kuwa mimi ningependelea wewe uvae nguo ipi, wakati nakujibu ulikuwa umepitiwa na usingizi ndiomana nikakupigia muda ule kukuambia kuwa nimependelea uvae gauni la pinki. Haya kosa langu ni nini hapo?? Je tutaenda huko beach?" Nilibaki kimya nikijishangaa kuwa usiku nilikuwa nikijadili na Sam kitu cha namna ile, Sam alingoja jibu hadi akaamua kukata simu.

Nilitafakari mara mbili mbili na kujiuliza sana kuwa au sikuota chochote sema ni maruweruwe tu, ila kumbukumbu zinaniambia kuwa mambo yale nimeyaona kwenye ndoto kwahiyo sikuwa na jinsi zaidi ya kukataa ile safari.
Sam aliponipigia tena nikamwambia kuwa sitaenda basi aliongea maneno mengi ya hasira. Kwakweli Sam alichukizwa sana na maamuzi yangu ila nilifanya vile ili kuepusha kutokea kama kilichotokea kwenye ndoto.
Mama akaja kunifata tena chumbani na kunikuta nikiongea na simu huku nikimbembeleza Sam aweze kunielewa.
"Simu hizo simu mwanangu, sijui hata zinakusaidia nini? Toka useme unaenda kuoga hadi sasa jamani? Hujala wala hujafanya chochote cha maana. Kwakweli nakuhurumia mwanangu, haya njoo tule chakula tayari mamako nishapika na kukuandalia malkia wa nyumba hii"
Mama akatoka, kwakweli nilijisikia vibaya ila ikabidi nitoke kumfata mama pale mezani ili asiseme tena.

Wakati tunakula, sauti ya Sam ikawa inajirudia kichwani mwangu kuwa kwanini nimemkatalia ile safari.
Sauti ile ikarudia mara kwa mara hadi nikajikuta nagonga meza na kusema,
"Aaaaaaaarggghhhhhhh........"
Kumbe nilipiga kelele mi nilijua kuwa nimejisemea chini chini, mama akashtuka na kuniangalia kwa jicho kali,
"Wee mwana wee umeanza kuwehuka?"
Nilibaki kumkodolea tu macho mama bila ya kusema chochote.
"Mamako nimepika chakula kizuri na kitamu ili malkia wa humu ndani ule ufurahi sasa unaniletea uchizi mezani. Unatatizo gani jamani mwanangu mzuri Sabrina?"
Nilitamani kumueleza mama ila nikajua kuwa kwa vyovyote vile lazima atazidi kumchukia Sam, ikabidi nimwambie kuwa sina tatizo. Ila kile chakula nilikuwa nakitazama tu na kuchezesha kijiko, mama alimaliza kula na kuniacha mwenyewe pale mezani. Badae nikaenda kukifunika jikoni, kisha nikarudi sebleni na kuweka picha za ngumi kwenye video na kuanza kuangalia.
Nikasikia simu yangu inaita, nikaenda kuichukua nikakuta ni Lucy ananipigia nikaenda kuongea nayo sebleni.
"Jamani Sabrina! Yani shem anakuomba mtoke out unamkatalia jamani! Kwani unafanya nini hapo kwenu?"
"Kwani wewe nani kakwambia?"
"Nimewasiliana na shem kaniambia, kwakweli ulichofanya sio kizuri shoga yangu."
"Fanya yako mengine hayakuhusu"
Halafu nikaikata ile simu hata nikajishangaa kwa kumchukia hadi Lucy.

Niliangalia Video ile ila bado haikunoga, moyo wangu ulikuwa unavutika kuwa ufukweni tu mambo mengine yote kwangu niliona kama ni kujisumbua tu.
Mama alikaa na mimi na tukaangalia wote ila bado haikunoga, hadi dada anarudi alinikuta palepale sebleni na sielewi chochote.
Mara gafla kichwa kikaanza kuniuma, nikamwambia mama akaenda kuniletea dawa nikanywa kisha akaniambia kuwa nikapumzike kwanza ilikuwa kama mida ya saa kumi na mbili jioni.

Nilipofika tu kitandani usingizi ukanichukua hapohapo na kama kawaida ndoto za maruweruwe zikanianza tena.

Nilikuwa mahali nimesimama na mbele yangu amesimama Sam huku akinilalamikia kuwa kwanini nimekaa kwenda nae.
"Najua Sabrina hunipendi ndiomana umekataa kutoka na mimi."
Na mimi nikamjibu,
"Hapana Sam nakupenda tena sana tu"
"Sabrina hunipendi, ila kuna mvulana mzuri na mtanashati wa kwenye ndoto zako ndio unayempenda. Najua yeye anaweza kukupa gari, nyumba na chochote cha gharama utakacho ila mimi sina uwezo huo Sabrina ndiomana hunipendi"
"Si kweli Sam nakupenda wewe"
"Ungenipenda mimi usingekataa kwenda beach na mimi Sabrina, usingekataa kutoka na mimi"
pembezoni mwa mazungumzo yetu akatokea yule kaka wa kwenye ndoto huku akitabasamu.
Nikashtuka gafla na kusema,
"Nakupenda sana Sam"
Kisha nikainuka pale kitandani, nikatoa gauni langu la pinki tena bila hata ya kufikiria mara mbili, nikavaa na viatu navyo nikavaa.
Kisha Nikatoka chumbani na kupita sebleni hakukuwa na mtu yeyote yule, wote walikuwa wameshalala kumbe ilikuwa ni usiku sana ila sikujali, nikaenda kufungua milango ili nitoke nje niende huko ufukweni.

NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 4:

Nikaenda kufungua milango ili nitoke nje niende huko ufukweni.
Nilikazana kufungua mlango wa nje bila ya kujari chochote na nikafanikiwa kutoka nje kumbe mama alisikia wakati nafungua milango, akatoka chumbani kuja kuangalia akaniona nikikazana kuongoza njia.
Mama hakujali kama alitoka na khanga moja ila alinikimbilia na kunishika mkono huku akianza kunirudisha nyumbani kwa nguvu ambapo nilikuwa nagoma.
"Jamani Sabrina mwanangu unaenda wapi?"
"Niache mama, naenda beach."
"Beach usiku huu mwanangu!! Nakuomba turudi nyumbani"
Nilikuwa nagoma kurudi, mama aliendelea kunivuta na dada Penina akaja kumsaidia mama ila kwavile nilipofika hapakuwa mbali sana na nyumba yetu, mama na dada walifanikiwa kunivuta na kunirudisha tena ndani kisha dada akafunga milango halafu mama akanipeleka sebleni na kunikalisha kwenye kochi.
"Mwanangu Sabrina jamani umechanganyikiwa?"
Nikawa namuangalia tu mama tena kwa macho ya hasira, dada naye akadakia.
"Hiyo beach ya usiku huu ukakutane na nani jamani mdogo wangu?"
"Hapo sasa, usiku huu akutane na nani? Mbona unataka kutuletea majini wee mtoto, hujui kuwa ndio mida yao hii? Tena huko baharini ndio nyumbani kwao"
Wakati mama akisema hayo mimi nilijiinamia na kuanza kulia bila sababu tena nililia sana.
"Nadhani fahamu bado hazijamrudia huyu"
"Hivi kwani ilikuwaje mama?"
"Nadhani kaamshwa na zile ndoto za usiku za kutembeza watu, si unazijua zile ndoto. Mtu anaamka na kwenda asipopajua na wengi hupotelea huko, jamani mwanangu kidonda cha babako hapa bado hakijapona halafu wewe unataka kunipatia kidonda kingine. Nitakuwa mgeni wa nani mimi jamani!!"
Mama aliongea kwa uchungu hadi nikaacha kulia na kumtazama usoni.

Mama alikuwa ananiangalia kwa sura ya huruma na upole sana.
Kisha akainuka na kwenda kuchukua maji na kuninawisha uso, kisha akaniinua na kunipeleka dirishani, akafunua pazia na kuniambia.
"Angalia giza la nje mwanangu, ni giza totoro na je unajua ni muda gani saizi?"
Nikatikisa kichwa kwa kukataa kuwa sijui.
"Ni saa nane usiku mwanangu, mbona unataka kuniletea makubwa wewe!"
Tulirudi na kukaa tena kwenye kochi huku akili yangu ikianza kama kuwa sawa hivi.
"Itabidi niwe nalala na funguo siku hizi naona mwanangu Sabrina ameanza kupatwa na vitu vya ajabu, maana mchana ameshindwa kula na usiku huu anataka kutoka bila taarifa mmh sijui ni mambo gani haya?"
Dada akashauri kuwa turudi kulala na mengine tuyazungumze kesho.
Basi mama akanipeleka chumbani kwangu na kuhakikisha nimepanda kitandani ndio akatoka na kwenda chumbani kwake.

Sikuweza kulala kabisa wala kujielewa, nilikuwa najishangaa tu. Kila nikiwaza nakosa jibu kabisa, yule mkaka mtanashati alishaichanganya akili yangu na sikujua kwanini alipenda kunifata kwenye ndoto zangu.
Kulipokucha, mama alikuwa wa kwanza kuja chumbani kwangu kuniangalia na kuniuliza kuwa nimeamkaje, ila nilikuwa mzima wa afya na nilikuwa Sabrina wa kawaida na siku zote.
Nilitoka na kuanza kufanya usafi ili mama atambue kwamba ninajielewa na wala hakuna tatizo tena kwangu.

Baada ya zile kazi mama akaanza kuzungumza na mimi kuhusu ndoto.
"Sikia nikwambie mwanangu, ndoto ni muunganiko wa mambo yote uliyoyafanya siku nzima, usiku ndio yanageuka na kuwa ndoto. Au mara nyingine ni mawazo unayoyawaza ndio hugeuka na kuwa ndoto"
Nikajifikiria inamaana mimi naota vitu ninavyoviwaza au.
Nikaamua kumuuliza mama,
"Inamaana mtu akiota ndoto ya kitu ambacho hajawahi fanya wala kuwaza inakuwa ni ndoto ya aina gani?"
"Mwanangu ndoto zingine hazitabiriki kabisa ila unachotakiwa kufanya ni kumuomba Mungu sana. Lakini mara nyingi ndoto huwa katika mtindo huo niliokueleza, kama vile wewe ulivyoamka usiku na kutaka kwenda beach inaonyesha hicho ni kitu ambacho ulikiongelea kabla"
Nikawa kimya kutafakari kauli ya mama kama ina ukweli wowote ndani yake.

Siku hii sikujishughulisha na simu kabisa nilikaa na kutafakari maisha yangu tu.
Ila ilipofika jioni nilichukua simu yangu kuangalia kama kuna mtu yeyote aliyenitafuta, nikaona hakuna ujumbe wala simu ambayo haikupokelewa.
Nikajiuliza kuwa inamaana Sam amechukia kiasi kwamba ameshindwa kunitumia hata ujumbe! Nikaamua kumtumia mimi mjumbe mfupi wa kumsalimia na ilionyesha kuwa umepokelewa ila hakukuwa na majibu kabisa, nikashangaa sana kwani tabia ya Sam imebadilika.
Kwa kawaida Sam hata nimkosee vipi hawezi kukaa kimya kunijibu hata salamu tu, nikaona lazima kuna tatizo hapa.

Muda huo nilikuwa chumbani na nikamsikia mama kapata ugeni wa rafiki yake pale sebleni, baada ya muda kidogo mama akaniita.
"Sabrina mwanangu, hebu njoo na huku uchangamshe akili"
Ikabidi nitoke nikakae pale sebleni na kumkuta mama Salome ambaye ni rafiki sana wa mama, nikamsalimia na kukaa. Yule mama akaendelea kuzungumza mazungumzo ambayo alikuwa anaongea na mama, ila mimi ndio nikawa mfano katika mazungumzo yake.
"Basi mtu mwenyewe yupo kama Sabrina, yani mwili wake hivyo hivyo. Akapandisha yale majini na kuanza kuropoka mambo ya pale"
Nikajikuta nikichukizwa na zile stori kwani sikupenda kusikiliza stori za majini karibia na usiku sababu zilinitisha wakati wa kulala, nikajaribu kuingizia mambo mengine kama vile kuwaulizia wakina Salome ila yule mama hakuacha kuelezea ile habari yake.
"Yani hali ilikuwa mbaya, kwakweli majini si ya kuchezea mama Penina"
"Sasa mkafanyeje?"
"Mwenzangu, si akataka tumtafutie marashi...."
Sikutaka hata kusikiliza zaidi, nikainuka na kurudi chumbani hadi pale niliposikia kuwa yule mama kaondoka.

Dada Penina aliporudi alikuja moja kwa moja chumbani kwangu.
"Kwani una tatizo gani mdogo wangu?"
Nilitamani kumueleza kuhusu zile ndoto ila nikasita.
"Sina tatizo dada"
"Basi njoo nikuonyeshe kitu"
Nikafatana na dada hadi chumbani kwake.
Akafungua mkoba wake na kunitolea maua mazuri sana na mdori mdogo mzuri,
"Umeona huyu mdori mdogo wangu na haya maua?"
Nikaitikia kwa kichwa.
"Kuna mtu kazini amenipa kama zawadi ila mimi nimeamua kukuletea wewe mdogo wangu, usiwe na mawazo sana. Unaweza kuweka hivi vitu mezani kwako na ukavifurahia"
Kisha nikaenda nae hadi chumbani kwangu, akanipangia yale maua na yule mdori kwenye meza ya pale chumbani kwangu.
"Umeona ilivyopendeza?"
Nikaitikia kwa tabasamu na kumshukuru dada kisha nikamkumbatia.
"Usijari mdogo wangu, sipendi kukuona na mawazo muda wote. Wewe bado mdogo, usijikomaze kwa mawazo. Ukiwa na tatizo lolote niambie hata kama litamuhusu Sam, mi kama dada yako nitakupa ushauri mzuri"
Nikafurahi ila wazo la kuwa Sam hajajibu ujumbe wangu likanijia kichwani na kujikuta nikinyong'onyea kiasi na kumuuliza dada.
"Hivi kwa mfano umemtumia message mtu unayempenda halafu hajakujibu utajielewaje?"
"Kwa haraka haraka unaweza kuhisi amekudharau au kuna kitu bora anafanya kuliko wewe ila ukweli ni kwamba simu haina vocha au imeharibika au ujumbe hajauona, usipende kumfikiria mtu kinyume. Sawa?"
Niliitikia kwa kichwa ila maneno yake yalinipa faraja kiasi.

Usiku wa leo baada ya kula, dada aliweka picha ya ngumi na kunitaka tuangalie wote. Tuliangalia hadi saa tano usiku kisha kuamua kwenda kulala.
Nikiwa kitandani, niliyatafakari sana yale maneno ya dada kuhusu kutokujibiwa ujumbe wangu hadi muda ule. Nikamtumia ujumbe tena na tena Sam ila bado sikujibiwa.
Niliendelea kuhisi kuwa Sam amenifanyia kusudi kwa kutokunijibu nikajisemea kuwa lazima kesho yake niende kwa Sam ili nikamuhoji.
Niliwaza na kupitiwa na usingizi pale kitandani.

Leo katika ndoto, nilimuona dada yangu akiwa kazini kwake kisha akatokea yule mkaka mtanashati wa kwenye ndoto zangu na kumkabidhi zawadi, dada alitabasamu na kuifungua yalikuwa maua na mdori kisha yule mkaka akanitazama mimi kwenye ndoto na kutabasamu.

Nikashtuka pale kitandani na jambo la kwanza lilikuwa ni kuangalia vile vitu alivyonipa dada, ile kupiga jicho kwa mdori nikamuona akitabasamu.
Niliogopa sana, nikajifunika shuka gubigubi ila bado nilimuona mdori yule akitabasamu.
Niliogopa hata kunyanyuka pale kitandani na kupiga makelele pia nilishindwa, nilijikuta nikiwa vile hadi kunakucha na palipokucha jambo la kwanza nilikimbilia chumbani kwa mama. Mama naye akashtuka na kuniuliza,
"Kwani kuna nini mwanangu?"
"Hata sijui"
"Na mbona umekimbia sasa? Si bure umeshaanza kuwehuka wewe."
"Hapana mama"
Sikutoka chumbani kwake hadi na yeye alipotoka, dada Penina alikuwa ameshaenda kazini.

Niliporudi tena chumbani kwangu hali ilikuwa shwari na yule mdoli alikuwa kawaida kabisa ila nikaamua kukusanya yale maua na yule mdoli na kuvirudisha chumbani kwa dada, kisha nikarudi na kukipanga chumba changu upya.

Mchana wa siku hiyo nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea Lucy, mama hakupinga akaniruhusu kwani alimuona Lucy nae aliponitembelea.
Safari yangu ilikuwa moja kwa moja hadi nyumbani kwa Sam, sikumkuta ila nikaamua kumngoja na hakukawia sana akawa amerudi kwenye mida ya jioni hivi.

Tukaingia ndani na kuanza mazungumzo, nilimlalamikia kwanini hajibu meseji zangu akadai kuwa hajapata ujumbe wangu hata mmoja na kusema kila alipojaribu kunipigia alikuwa hanipati hewani.
"Yani hapa nilikuwa nafikiria Sabrina kuwa nimekukosea nini hadi kufikia hatua ya kunizimia simu? Wakati kama safari ya beach ulikataa mwenyewe"
Kwakweli sikumuamini Sam kama kweli alikuwa hanipati hewani wakati simu yangu ipo hewani muda wote na sikumuamini kama kweli meseji zangu hazikufika kwake wakati kwangu zilionyesha kuwa zimefika.
Nikamnyang'anya simu yake ili kuhakikisha kama kweli na moja kwa moja nikaenda kwenye ujumbe unaotumwa kwake (inbox), kuangalia kama kweli ujumbe wangu hata mmoja haukufika.
Kwakweli wakati naangalia nikapatwa na presha kabisa kuona ujumbe uliotumwa na Lucy ukiwa umeongozana kwenye simu ya Sam, tena kila ujumbe niliosoma ulikuwa ni mzito sana.

Nilimuangalia Sam kwa jicho kali sana,
"Ndio nini hiki Sam?"
"Kwani nini?"
Nikampa ile simu yake aangalie mwenyewe.
"Angalia upuuzi unaochat na Lucy"
"Jamani! Lucy si rafiki yako na umenitambulisha mwenyewe?"
"Sasa kama rafiki yangu ndio uchat nae message za namna hiyo?"
"Kwanza unanipa lawama za bure Sabrina na unapandisha jazba bure tu. Tulia kwanza nikueleze"
"Hakuna cha kunieleza Sam, ujumbe wa humo umeshajitosheleza. Sam wewe una tamaa sana yani hadi kwa rafiki zangu loh!"
Nikainuka na sikutaka maelezo yoyote ya ziada na kuanza kuondoka kwani nilipandwa na hasira za ajabu.
Sam akawa ananirudisha ila sikutaka kumsikiliza wala nini ndio kwanza niliongeza mwendo.

Sam alinifatilia hadi alichoka na giza lilikuwa limeshatanda, akaomba kunisindikiza nyumbani nikamkatalia sikutaka tena kumsikiliza Sam ikabidi aniage kwa lazima huku natembea haraka haraka akasema kuwa kesho atakuja nyumbani ili tuweze kuzungumza vizuri.
Sikumsikiliza chochote na niliendelea na safari, nilifika kwenye njia flani na haikuwa na mtu yeyote, nikasikia nyuma yangu mtu akiita,
"Sabrina"
Nikapatwa uoga hadi nikashindwa kugeuka kwani sauti ilikuwa ya kiume ila sio ya Sam.
Wakati natembea haraka haraka nikahisi kama huyo mtu ananikimbilia kwa nyuma, nami nikaanza kukimbia. Nikasikia tena sauti,
"Usinikimbie Sabrina, usiogope."
Nikazidi kupatwa na uoga kwani yule mtu alishafika nyuma yangu.
Mara akanishika bega, uoga ukazidi kunijaa kwani mikono yake ilikuwa na ubaridi uliopenya mwilini mwangu.

NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA 5:

Uoga ukazidi kunijaa kwani mkono wake ulikuwa na ubaridi uliopenya mwilini mwangu.
Nilishindwa kugeuza shingo yangu kumtazama kwani nilijua wazi atakuwa ni yule jamaa wa kwenye ndoto zangu, jamani kwenye matatizo acheni kabisa kwani gafla nilitoa mbio hata nadhani ingekuwa ni mashindano basi lazima mimi ningekuwa mshindi.
Mbio nilizokimbia haikuwahi kutokea maishani mwangu, nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa na kujikuta gafla nishafika kituo cha madaladala huku nikihema juu juu.
Ikatokea daladala mbele yangu na kuisimamisha, iliposimama nikapanda na kukaa kwenye siti. Nikajiinamia chini, sikujielewa kabisa na sikuelewa chochote.
Nilipokaribia na kituo cha nyumbani nikatoa nauli na kumwambia konda ashushe, gari iliposimama nikashuka na kuanza kuondoka mara konda wa daladala akanishika bega na kusema,
"Umesahau chenji yako Sabrina"
Nilihisi kupagawa kwani mkono wa yule konda ulikuwa na ubaridi kama wa yule mtu aliyenishika bega njiani, na je yule konda amejuaje jina langu? Nilihisi kuchanganyikiwa, nilipogeuka kumuangalia yule konda nikamuona akitabasamu kama yule mdoli.
Hapo nilihisi kuwa chizi jamani kwani nilianza kukimbia huku nikipiga makelele ya kuomba msaada, nilikimbia na kituo cha kwanza ilikuwa ni nyumbani kwetu. Nilifika mlangoni na kuanguka na kupoteza fahamu kabisa.

Nilipozinduka nilikuwa mikononi mwa mama, kichwa changu kilikuwa kwenye mapaja yake. Kumtazama usoni alikuwa amejawa na machozi huku dada akiwa pembeni na mama Salome.
Niliinuka ili niweze kukaa, mama akanisaidia kufanya hivyo kisha wakanipa maji niweze kunywa.
Baada ya kutulia, mama akaanza kuniuliza.
"Umepatwa na nini mwanangu? Unajua umenitisha!"
"Mmh hata sijui nimepatwa na nini mama ila viungo vyangu vyote vinauma"
Mama akaniambia kuwa ilibidi wamuite mama Salome ili kunipatia huduma ya kwanza kwani yeye alikuwa ni nesi mzoefu. Na ndiye aliyewapa moyo kuwa nitaamka tu.
Siku hiyo nililala chumbani kwa mama kwani mama alitaka kuangalia hali yangu inaendeleaje kwanza.
Kabla ya kulala nilienda kumuuliza dada maswali mawili matatu wakati anatizama video.
"Eti dada kwa mfano ukahisi mpenzi wako amekusaliti, je kuna haja ya kusikiliza maelezo yake?"
"Sikia mdogo wangu, unapomuhisi mpenzi wako vibaya au unapoona kitu kibaya toka kwake hutakiwi kufanya hasira. Unachotakiwa kufanya ni mambo matatu, kwanza kabisa muulize mpenzi wako kuhusiana na kile unachohisi, kusikia au kuona, pili sikiliza maelezo yake hata kama anakudanganya na tatu kaa chini kutafakari na kuyapima maelezo hayo. Usipende kuchukua maamuzi ya gafla kwani yatakuumiza wewe na umpendae"
Ushauri wa dada ukaniingia na kunikaa sawa, kisha nikaenda kulala huko kwa mama kwani mama alikuwa ameshalala muda huo.

Kesho yake nilikuwa na hali ya kawaida kabisa na kuanza kuongea na kucheka na mama.
"Ila wewe mwanangu ni wa ajabu, sijui ulifukuzwa na wezi jana. Yani umekuja na mbio na kuangukia mlangoni, pochi yako ndogo mkononi na simu ndani ya pochi mmh mi nilijua umevitupa"
Kwanza na mimi nilicheka kwani nikikumbuka jinsi nilivyokimbia halafu bila kutupa ile pochi ni kitu cha ajabu sana.
"Mambo mengine ni maajabu tu mama yangu"
"Ila nini kilikukimbiza haswaa?"
"Kuna mtu alinitisha pale stendi, ndiye aliyefanya hadi nianze kukimbia."
"Una vituko wewe, ulinitisha sana ujue"
Niliongea mambo mengi ya hapa na pale na mama.

Mchana wa siku hiyo Sam alifika nyumbani na kumkuta mama, kiukweli mama yangu alikuwa hampendi Sam ila Sam anapofika na kuniulizia mama lazima ataniita ila atanipa muda wa kuzungumza nae.
Mama akanifata ndani,
"Sabrina, kijamaa chako kipo hapo nje kinakuulizia. Sasa sio ndio unachukua muda wote kuzungumza nae, ongea nae kidogo arudi kwao. Sawa?"
"Sawa mama"
Aliposema tu kijamaa nilijua moja kwa moja anamzungumzia Sam.
Nikatamani kukataa kwenda kuzungumza nae kwa yale ya jana ila pia nilitaka kujua anajipya gani la kujitetea kwani nilifata ushauri ambao dada alinipa.

Nikatoa viti viwili na kukaa nje na Sam, na yeye alikuja kutimiza ile azma yake ya jana kuwa angekuja leo nyumbani kwetu na ndio alikuwa amekuja.
Nilikuwa najiandaa kusikiliza maneno ambayo Sam angeongea kujitetea, hata hivyo nilijua lazima atakachoongea kitakuwa cha uongo tu.
"Sam, hivi unajua jinsi gani nakupenda? Na je unajua ni jinsi gani nimeumizwa na huo uchafu wa kwenye simu yako?"
"Naelewa mpenzi ila unatakiwa kunisikiliza kwanza ili nikwambie ilivyokuwa, na unachofikiria juu yangu si kweli"
"Haya, ongea huo ukweli"
"Siku ile uliyowasiliana nami kwa kutumia ile simu ya rafiki yako, badae alinitafuta na kusema kuwa ananisalimia. Nilishamsahau ila alipojitambulisha ndio nikagundua kuwa ni rafiki yako wa mchana.
Kesho yake akanipigia simu asubuhi na kunisalimia, kisha akauliza kuwa nina mipango gani siku hiyo. Nikamwambia kuwa nimepanga kwenda beach na wewe, akaniambia ni vizuri kisha akapongeza kwa hilo.
Badae akaniuliza kama tumeshaenda huko beach, nikamwambia kuwa wewe umekataa ndio akasema kwamba atajaribu kuzungumza na wewe."
"Kwahiyo zile message alikuwa akikufariji kwavile mimi nimekataa?"
"Bado sijamaliza maelezo mpenzi"
"Haya, malizia basi"
"Badae akanipigia simu na kusema kuwa wewe unaonekana kuna kitu umechukizwa na mimi, hivyo akaniambia kuwa anao ujumbe wa kutosha wa mapenzi unaoweza kukufariji wewe, ndio akaanza kunitumia zile message kuwa niziangalie nikiona inayovutia nikutumie wewe. Ila mi sikuwa nachat nae na wala sikumuomba hizo message"
"Kwahiyo ulitaka mimi nifarijike kwa maneno ya mwanamke mwenzangu? Ulishindwa vipi kumzuia asikutumie? Nadhani ulizipenda ndiomana hukuziondoa kwenye simu yako."
"Si kweli Sabrina, yule ni rafiki yako. Mimi siwezi kukusaliti na kuwa na rafiki yako au kuwa na msichana mwingine, wewe ndiye nikupendae"
"Kweli nimeamini kuwa wanaume ni waongo, yani Sam message inasema nimekumiss sana baby na mwishoni anamalizia na busu mmwaaaaaah halafu unataka kuniambia ni mimi tu unipendaye?"
"Nielewe Sabrina nilichokwambia ni ukweli mtupu, au basi niambie cha kufanya ili upate kuniamini tena. Nakupenda Sabrina"
"Ngoja nifikirie kwanza maelezo uliyonipa kama yana ukweli wowote, ila nisingependa kuona ukiwasiliana tena na Lucy. Nadhani tumeelewana"
Sam alionyesha kujutia sana kile kitendo cha mimi kukuta jumbe za Lucy kwenye simu yake ila ndio hivyo maji yakimwagika hayazoleki.
Nikaagana pale na Sam akaondoka zake tena si kwa kawaida yetu ya kusindikizana, nilimwacha aondoke mwenyewe kama alivyokuja.

Mama akanishangaa kuwa mbona sijamsindikiza Sam.
"Kheee malkia leo umemuacha mfalme wako kaondoka mwenyewe!! Kulikoni??"
"Hakuna kitu mama"
"Mmmh hakuna kitu kweli? Ila kama mmeachana basi ashukuriwe Mungu"
Akainua na mikono juu kuonyesha shukrani hadi nikajisikia kucheka.
"Kwanini mama humpendi Sam?"
"Sio type yako, haendani na wewe kabisa. Wewe mwanangu unatakiwa kupata mwanaume wa ukweli, mwenye kazi ya maana na pesa zake halafu msomi ila sio hao vidampa kama huyo Sam"
"Ila mama mapenzi sio pesa"
"Usibishane na watu tuliotangulia kuliona jua, je utapenda kuona watoto wako wakipata shida au raha?"
"Napenda wanangu wafurahi"
"Basi fata ushauri wangu, olewa na mtu anayejielewa utaona faida yake"
Anavyoongea mama kama vile Sam nae hajielewi wakati Sam ni mwanaume anayejielewa na kujitambua pia.

Dada aliporudi, aliniita chumbani kwake na sikujua ameniitia kitu gani.
Kumbe aliniita kuhusiana na vile vitu ambavyo nilirudisha chumbani kwake.
"Mbona umerudisha maua na mdoli ambaye nilikupa? Nilitaka kukuuliza jana sema ndiovile hukuwa na hali nzuri"
"Me sivitaki tu dada ndiomana nimekurudishia"
"Hadi mdoli Sabrina! Inamaana siku hizi hupendi tena wadoli?"
"Mi sijisikii kuwa navyo tu dada"
"Basi hakuna tatizo vitakaa humu chumbani kwangu"
Sikuweza kumwambia dada ukweli kama yule mdoli alikuwa akitabasamu.

Tulipokaa sebleni dada akamwambia mama kuwa aliniletea zawadi ya mdoli na maua ila nimevirudisha nakudai kuwa sivitaki.
"Ukiona hivyo ujue amekua, maswala ya madoli hayo ni mambo ya kitoto tu. Angekuwa kijijini Sabrina usikute angekuwa na watoto hata watatu sasa hivi"
Dada na mama wakawa wanacheka,
"Nimemshangaa sana leo kukataa mdoli kweli amekua mdogo wangu, eti Sabrina au ndio Sam anataka kukuoa?"
"Atakaemuozesha kwa huyo Sam ni nani? Labda nife ndio aolewe nae"
Kwakweli kauli za mama juu ya Sam hazikuwa nzuri kabisa, ila leo hawakuzungumzia zile stori zao za kutisha angalau nyumba ikawa na amani.

Hata mi mwenyewe, Leo nilikuwa na amani na kwenda kulala chumbani kwangu, kwanza kabisa nilizungumza na Sam kwenye simu kisha nikalala kwa amani kabisa.

Nikawaona Sam na Lucy wakiwa kwenye penzi zito huku mimi roho ya wivu ikiniuma, waliendelea na mapenzi yao na mwisho wa siku wakafunga ndoa.
Nilishtuka sana na jasho jingi likanitoka, yani Sam ananiongopea? Kumbe kweli ana mahusiano na rafiki yangu Lucy hadi watafikia hatua ya kuoana, roho iliniuma sana.
Wakati nawaza hayo, usingizi ukanichukua tena.

Yule mkaka mtanashati akanionyesha nyvmba nzuri sana na kusema kuwa itakuwa mali yangu endapo nitakubali kuwa na yeye, akanyoosha mkono wake ili niambatane nae lakini mimi nilikataa, akawa anafanyakazi ya kunisogelea huku akitabasamu na mimi nikazidi kusogea nyuma, nikafika mahali nikawa nimekwama, kuangalia nyuma kulikuwa na shimo refu lenye wadudu wengi na mbele yangu ni yule mkaka aninisogelea, nilipotaka kuanguka kwenye lile shimo nikashtuka na jasho liliendelea kunitoka tena jingi kushinda la mwanzo. Nikajiuliza kuwa hii ndoto inamaana gani nikakosa jibu.

Nikabanwa na haja ndogo na kuinuka pale kitandani ili niende chooni.
Choo chetu kilikuwa ndani, ila nilipokaribia mlango wa choo nilasikia kama mtu anacheka nikajiuliza ni nani usiku ule wakati mama na dada walikuwa wamelala.
Kufika kwenye mlango wa choo nikamkuta yule mdoli akiwa mlangoni na uso wake ulitazama kwangu huku ukitabasamu, nikaanza kuogopa nikatamani kupiga kelele ila nilishindwa nikaamua kukimbilia chumbani huku nahema juu juu kwani ni mambo ya ajabu ambayo sikuyatarajia kabisa. Nikabamiza mlango kwa uoga.

Nikiwa chumbani kwangu nikaanza kujilaumu kuwa kwanini sikwenda chumbani kwa mama moja kwa moja ila niliogopa kutoka tena.
Nikakaa kitandani kwa uoga, gafla nikashikwa na kitu mgongoni ile kugeuka na kuangalia ni yule mdoli wa chumbani kwa dada, alikuwa akitabasamu kama yule mkaka wa ndotoni.
Hali ilikuwa mbaya zaidi pale nilipotazama mezani na kumuona tena yule mdoli na yale maua.
Hofu ikanitanda, uoga ukajaa nikainuka pale kitandani ili nikafungue mlango nikimbilie chumbani kwa mama.
Nilipoufikia mlango, yule mdoli nae alikuwa mlangoni akitabasamu halafu kwa mbali nilisikia mtu akiita jina langu.

Itaendelea

Where do you want to donate?

Traktir Kopi
Bank BCA - An. Asep Saepul Anwar/ Rek - 648xxxx
Treat the creator to coffee by giving a small donation. click the arrow icon above

Chapisha Maoni

Copyright ©BongoLife - All rights reserved.

Redesign by bloggun.xyz
Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
More Details