UKURASA WA 56 SEHEMU YA 03

UKURASA WA HAMSINI NA SITA 
SEHEMU YA 3
Malocha akiwa haelewi wala kujua ni nini kinatokea nyuma yake, yeye alikuwa anakimbia kwa nguvu huku wazo la kuangalia nyuma likiwa halipo kabisa. 
Akiwa kavaa suti yake mwanana, tai ikiwa inapepea kurudi nyuma kutokana na upepo unaokuja sababu ya kukimbia, mara pikipiki aina ya Honda, mali toka Japan, toleo jipya kabisa, ilisimama mbele yake.

“Get over there if you wish to live.” Sauti mwanana ya kike ilisikika baada ya kusimama mbele ya Malocha huku akimuonesha na kumwambia apande sehemu ya nyuma ya pikipiki yake kama anataka kuishi.
Malocha hakuwa na namna, akafanya vile alivyoambiwa mbele ya mwanamke ambaye hajajionesha sura kwake bali kuvaa kofia ya kuendeshea pikipiki. 
Malocha naye akapewa kofia ya kuvaa, kisha kwa fujo zisizo na maelezo, mwanadada aliingiza gia kwenye pikipiki yake na kwa mbwembwe akanyanyua tairi ya mbele na kuitua chini kwa fujo na safari ya kunyoosha barabara ikachukua nafasi huku kijana wa Kitanzania akijaribu kutazama nyuma na kushuhudia waenyeji wake wakiwa hawaamini kama wamemkosa kibwege namna ile.
****
Baada ya kuambiwa akaribie kwenye ufalme wa kifo, General Pyong ni kama alikuwa kaambiwa sasa muue huyo mweusi mwenye nyodo. Aliruka kwa ustadi huku mguu mmoja akiutanguliza mbele na kuona hivyo, Masai akakwepa kwa kusogea pembeni huku akijisahau kuwa jamaa yule alikuwa kakamata visu vikali mikononi mwake na alivitumia vema kwa kukwangua sehemu ya mkono wa Masai lakini havikugusa nyama na badala yake vilikata koti la suti alilokuwa katinga mwilini.

Masai akiwa anajiangalia pale palipochanwa, Pyong akarusha teke kinyumenyume na kumbabatiza kijana wa Kitanzania kwenye kifua na kumfanya ayumbe kama mtu aliyeanza kulewa. Kijana shupavu akatafuta balansi kwa kugota ukutani na kisha akamtazama mpinzani wake ambaye alikuwa kadhamiria kumaliza mpambano bila kuguswa ngumi hata moja.

Visu viwili alivyokuwa kavikamata mkononi, vikawa tayari kwa kuchoma kifua cha Masai ila haikuwa hivyo kwa sababu tayari mwanaume alikuwa kaviona na kukwepa kidogo kisha akamsukuma mgongo yule bwana na kufanya vile visu vichome uzio au tuseme ukuta wa chumba kile ambao ulikuwa umejengwa kwa maboksi/makaratasi. 
Baada ya kitendo kile, Pyong akageuka haraka huku kwa nguvu akivurumisha mkono wake wa kulia tayari kwa kumchana Masai maeneo ya kichwani ama akikosa huko amchane shingoni. 

Bahati haikuwa yake tena, Masai alichutama kidogo na mvumo ule wa mkono wenye kisu ukapita juu yake na wakati huohuo, akifyatua ngumi yake kali iliyokita kwenye mbavu za Pyong. Mkorea akabwata kwa sauti ya maumivu na kushika eneo llilokumbwa na dhahama ya ngumi nzito ya Kitanzania. 
Kabla hajaendelea kuuguza maumivu hayo, alishtukia konde lingine la shavu likitua na kumtemesha damu nzito iliyochanganyika na udenda. Pyong akajikuta kwenye wakati mgumu sana hasa pale alipopigwa ngumi iitwayo ‘kata funua’, yaani inatokea chini na kutua kidevuni. Ngumi hiyo inaweza kukuvunja taya kama itapigwa kiustadi zaidi lakini kwa Pyong ilimpa maumivu makali sana.
Akiwa anayumbayumba baada ya kichapo kizito, Masai akaruka angani na kumpiga teke la kuzunguka (Round Kick) ambalo nalo liliendelea kumpiga maeneo ya mdomoni. Kijana wa Kitanzania alipoona kamnyong’onyeza Mkorea, akaruka tena lakini safari hii alitanguliza miguu yote miwili mbele na yote kwa pamoja ikakita kwenye kifua cha Pyong na kumrusha hadi kwenye kuta za makaratasi na kuzichana kabisa. Pyong akawa hoi huku akiwa haamini pamoja na uwezo wake wa kupambana anaweza kupigwa na mtu kama Masai.

Kwa tambo nyingi, Masai akainama na kuchukua kisu kimoja cha Pyong alichokidondosha baada ya kichapo cha kufa mtu. Akawa anaenda pale alipodondokea Mkorea mwenye cheo na mamlaka makubwa jeshini, General Jing Pyong.

“Nilikwambia, huku unapopataka ni ufalme wa kifo. Unaona sasa?” Masai akaongea wakati alikwishafika alipokuwa amelala Pyong. “Sasa kataa au ukubali, ni lazima ufe. Halafu atakayefuata ni boss wako. Ndilo jina la kwanza limeonekana kwenye ukurasa wa hamsini na sita. Kwako nilitaka kujua tu! Nampataje boss wako?” Akauliza.

“Huwezi kumpata mbwa wewe. Heri nife.” Akajibu kwa dharau Pyong.

“Basi sawa. Hii hapa simu, utampigia mbwa wako na kumwambia naelekea kuiteketeza familia yake,” Maneno hayo yakaenda sambamba na Masai kurusha simu ya mkononi. “Lakini kabla sijaondoka, utamwaga damu ambazo zitakufanya ufe tu! Chaguzi ni lako.” Masai akashika mkono wa kushoto wa Pyong na kuchana ile sehemu iliyokaribu na kiganja cha mkono. 
Sehemu hii pia inapita mshipa mkuu wa damu na ndio maana ukienda hospitali kutundikiwa ‘dripu’, hupatumia hapo. Ni rahisi sana sehemu hiyo kutoa damu ambayo inaweza kusababisha umauti. “Ufe salama nguruwe. Msalimie malaika mtoa roho huko uendako.” Kwa maneno hayo yaliyotoka kwa lugha ya Kikorea, ni wazi Masa alikuwa amemaliza kazi ya kummaliza General Pyong. 
Kijana wa Kitanzani akatoka ndani ya chumba kile na kumuacha Pyong akiwa anatapatapa akijaribu kutafuta msaada wa huduma ya kwanza lakini ilimuwia vigumu sana. Mwishowe aliamua kuchukua simu na kumpigia Waziri wa Ulinzi Mstaafu wa kipindi hicho ambaye ndiye miaka mitano iliyopita aliongoza msako wa Chude Bobo huko Tanzania.

“Bosi, nipo mahututi. Yule kijana aliyechukua ukurasa wa hamsini na sita, kasema anakuja kwa familia yako. Kama kuna ulinzi, ongeza.” Baada ya maneno hayo, akakata simu na mara macho yake taratibu yakaanza kukumbwa na giza.
*****
Masai alipomaliza kumchana Pyong kwenye mshipa mkubwa wa damu, moja kwa moja akatoka nje huku kakamata kifaa kimoja kama simu ya kisasa, yaani ni kioo tupu mbele ya kifaa hicho. Akabonyezabonyeza na kisha kikawaka, akabonyeza namba zilizoonekana hapo na mara ikasikika kelele ya gari ambalo liliambatana na kuwaka taa. 
Lilikuwa ni gari la kisasa sana ambalo unaweza kuliwasha na rimoti. Bugatti Veyron, ndilo gari lililokuwa mbele ya Masai. Rangi yake ikiwa ni nyeusi na buluu. 
Gari hili linaweza kukimbia Mita 60 kwa sekunde 2.4 na kasi yake ya juu ni 248mph (Metre Per Hour). Pia lina turbo, kitu ambacho kinaweza kuifanya gari hili liende kasi zaidi kwa kuibusti injini. Ni gari matata na linakasi kubwa sana bila kusahau uwezo wa kipekee kabisa, wa kutumia nywila ili kulindesha.

Na sasa lilikuwa mbele ya macho ya Man’Sai ambaye alitetemeka baada ya kuliona. Hata alipotazama huku na huko, bado pia kuna watu ambao walimtolea macho na kutoamini kuwa kuna mtu mweusi anaweza kumiliki gari la namna ile. Ili kutopoteza muda na kutoonekana mshamba, aliingia ndani ya gari na gari nalo lilimuuliza jina lake kamili.

“Frank Masai.” Kijana akajibu na hapohapo gari likawaka kwa sauti iliyozidi kufanya umati wa watu kulitazama gari lile ambalo ndilo lina kasi labda kushinda magari mengi duniani.

“Una kazi ya kufanya Masai, kubwa sana,” Kioo cha gari lile, kiligeuka kuwa skrini kama ya video na sauti ilitoka mule ndani bila mtu kuonekana. “Kwanza weka simu iliyonasa maongezi ya Pyong na Waziri Mstaafu kwenye hiyo droo ya umeme.” Aliposema hayo, droo hiyo ikafunguka na Masai akaweka simu yake. Maongezi kati ya General Pyong na Waziri Wa Ulinzi aliyepita yakaanza kusikika. Baada ya kumalizika, ramani fulani ikatokea kwenye kioo cha gari lile ikionesha ni wapi sauti ilitoka na ilienda wapi. Yaani toka kwa Pyong kwenda kwa Waziri.

“Waziri huyu yupo nje kidogo ya Korea. Lakini si kitu, unatakiwa kumpata na kumfanya atubu dhambi zake zote. Amekwishapigia simu familia yake na kwake kumeongozeka ulinzi. Cha msingi ni kuhakikisha haondoki huko alipo sasa hivi. Ramani ya kukufikisha huko, hiyo hapo kwenye luninga ya gari.” Baada ya maneno hayo, luninga ndogo ya gari lile ilifunguka na ramani ikaonekana na aliweza kucheza nayo vema sana Masai kwa sababu ya usomi wake wa Jografia.

“Malocha yupo wapi?” Masai akajaribu bahati yake kuona kama yule mtu anayeongea naye yupo moja kwa moja au amenakiriwa tu.

“Yupo kwenye mikono salama kwa sasa. Anaelekea iliponyumba yenye ulinzi. Kesho atakuwa Tanzania.” Akajibiwa na hiyo ikawa ahueni kwake. “Swali lingine Masai?” Akaulizwa kwa lugha ileile ya Kiingereza.

“Twende kazini sasa.” Maneno hayo yakafanya kile kioo cha gari kuzima, na kijana wa Kitanzania akalitoa lile gari la gharama toka eneo lile.
****
Pikipiki aliyokuwa amepakizwa Malocha, ilikuwa inakata mitaa kwa kasi ya hatari. Huku wakiwa wapo katika kasi hiyo, Range Rover Sport, rangi nyeusi, iliibuka toka barabara za mkato na kuanza kuifukuza pikipiki ile kwa lengo moja tu! Kumkamata Malocha eidha akiwa mfu au hai.

“Shit! Wajinga hao nyuma yetu,” Aliongea mwanadada anayeendesha pikipiki na sauti hiyo Malocha aliisikia kwa sababu kofia aliyovaa ilikuwa na vinasa sauti vilivyokaa masikioni vema.
“Ni wakina nani hawa?” Akauliza Malocha.

“Hao ni maadui tu! Wanataka kujua Chude Bobo ni nini? Kifupi wanajua kuwa wewe unakila kitu ambacho kitawasaidia. Ni watu hatari sana hao. Kama wakikupata, watakutesa sana tu. Hapo wanachokijua kichwani mwao ni kwamba, Chude Bobo inaramani ambayo itawapeleka kwenye madini ambayo ni hatari kuliko yale ya kutengenezea nyuklia.” Akajibiwa.

“Sasa mbona kitabu chenyewe hakina ramani hiyo?” Akauliza tena.

“Wenzako hawajui, na watakuua kama utawajibu hivyo,” Akajibiwa tena. “Unajua kutumia bastola?” Mwanamke yule nguli wa kuendesha pikipiki, wala hakusubiri kujibiwa, akatoa bastola pembeni ya pikipiki yake na kumpatia Malocha. “Pambana nao.” Akapewa ruhusa Malocha ambaye naye hakujivunga kwenye kujichukulia sifa za kupambana. Akajigeuza kwa ustadi na kujikuta amempa mgongo mwendeshaji naye akiwa anaitazama ile Range Rover nyeusi inayowakimbiza. Akaanza kuifyatulia risasi na wale mabwana kuona hivyo wakapunguza mwendo ili wasikumbwe na dhahama.

“Sipendi bastola.” Malocha alijisemea lakini sauti ile ilisikika kwenye masikio ya suka anayeiongoza ile pikipiki.

“Chukua hii.” Akapewa bunduki aina ya ‘shotgun, M 180- D1 Spring Airsoft’.

“Oooh! That’s my baby.” Malocha aliipokea bunduki ile na kuibusu huku akiisifia kuwa ile ni mpenzi wake. Akaikoki tayari kwa kuwashambulia wale mabwana na wakati huo Honda Hayabusa, pikipiki aliyokuwa kapakizwa, ilikuwa inakata mitaa.

Where do you want to donate?

Traktir Kopi
Bank BCA - An. Asep Saepul Anwar/ Rek - 648xxxx
Treat the creator to coffee by giving a small donation. click the arrow icon above

Chapisha Maoni

Copyright ©BongoLife - All rights reserved.

Redesign by bloggun.xyz
Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
More Details