NAMTAKA MPENZ WANGU ARUDI SEHEMU YA 05

NAMTAKA MPENZ WANGU ARUDI
SEHEMU YA 5
WHATSAPP 0655585220
ZANZIBAR
Wanaume hawakutaka kuwa na subira, walichokifanya ni kuanza kumfuatilia kwa lengo la kumtia mikononi mwao lakini kwa Nandy, lilikuwa jambo gumu kumkubali mwanaume yeyote yule kimapenzi.
“Jamani yule demu mkali mno, ila naye mgumu kama nondo,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Nandy.
“Watu wamemfuata lakini wapi. Ana sauti nzuri ya kumtoa nyoka pangoni lakini ni mgumu sana, hivi kuna mtu anaweza kumpata yule?” aliuliza jamaa mwingine.
“Sidhani! Ila tupambaneni, mwenzenu mimi huwa siamini kama kuna demu mgumu, watu wanazaa na malkia anayewaongoza ndiyo sembuse yeye! Tuweni bize naye tu,” alisema jamaa mwingine.
Miongoni mwa wasichana aliowahi kutembea nao Dickson alikuwa Linda Fabian. Huyu alikuwa msichana mrembo aliyekuwa akisomea sheria nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Oxford.
Linda alikuwa miongoni mwa wasichana warembo ambao walitoka kimapenzi na Dickson. Katika kipindi ambacho wawili hao walikuwa pamoja walipeana ahadi nyingi za kuwa pamoja mpaka kuja kuoana.
Kwa mapenzi motomoto ambayo Linda alipewa na Dickson, moyo wake ulichanganyikiwa na kuona kuwa katika dunia nzima hakukuwa na mwanamke mzuri kama alivyokuwa.
Dickson hakuwa na mapenzi naye, alimuonyeshea kwa kuwa aligundua kwamba msichana huyo alichanganyikiwa kwake. Walikuwa pamoja, walifanya mambo mengi pamoja na hata wakati mwingine kwenda kutembea nje ya nchi.
Walipendana, kila mtu aliyekuwa akiwaangalia aliona kabisa kwamba wawili hao wangekuwa pamoja siku moja na kutengeneza familia pamoja. Linda alichanganyikiwa, akawaambia wazazi wake kuhusu Dickson kitu ambacho kwa kijana huyo hakupenda kabisa kuona kikitokea.
Penzi likawa wazi lakini bado Dickson alikuwa mtu wa wanawake, hakuwahi kupenda kwa moyo wa dhati, hakuwahi kumwambia mwanamke kwamba alikuwa akimpenda kutoka moyoni mwake.
Kwa uzuri wa sura aliokuwanao aliamini kwamba wanawake walimpenda wao wenyewe na kutaka kulala naye. Hakuwahi kutongoza, wanawake wote aliowahi kulala nao katika maisha yake akiwemo Linda walikuwa wakimtongoza yeye.
Alitembea na wanawake wengi, watoto wa kishua wenzake lakini mtu aliyekuwa karibu naye zaidi alikuwa Linda tu ambaye alimganda kama ruba.
Siku zikaendelea kukatika mpaka siku ambayo Linda alihisi hali ya tofauti mwilini mwake na alipokwenda kupima, akagundua kwamba alikuwa na mimba. Hilo lilimtisha,hakutaka kufanya siri, akamwambia Dickson ambaye aliruka kama ndege na kumwambia kwamba mimba haikuwa yake.
“Kumbe ni ya nani?” aliuliza Linda, kwa jinsi Dickson alivyokuwa amebadilika, hakuamini macho yake.
“Sijajua! Labda ya mwingine, huwezi kujua,” alisema Dickson.
“Kwa hiyo nilitembea na mwanaume mwingine?”
“Kwani mimba mpaka utembee na mwanaume, hujawahi kusikia mimba inayopatikana kwenye bwawa la kuogelea? Linda, mara ya mwisho nilikuuliza kama upo kwenye siku za hatari, unakumbuka ulinijibu nini?” aliuliza Dickson.
“Kwamba sikuwa kwenye siku za hatari!”
“Sasa mimba imeingiaje?”
“Dickson, sikujua kama mzunguko wangu ulibadilika,” alisema Linda.
Dickson hakutaka kukubali, hakutaka kuitwa baba kwa msichana ambaye hakuwa na ndoto zake. Wakaingia kwenye mtafaruku wa kimapenzi na baada ya kuona kuwa mwanaume huyo ameweka vikwazo, akaamua kuitoa mimba hiyo.
Moyo wa Linda ulimuuma lakini hakuwa na jinsi. Uhusiano uliendelea lakini Dickson hakuwa mtu wa kueleweka tena, wakawa kama marafiki, hakuwa mtu wa kumpigia simu Linda na kumjulia hali, kwake, hakutaka kabisa kuwa na mapenzi na msichana huyo.
Maisha yaliendelea kama kawaida mpaka Linda alipoamua kuondoka na kuelekea nchini Uingereza kusoma. Kwake, Dickson alikuwa kila kitu, hakutaka kuona akimpoteza mwanaume huyo, japokuwa aliona kabisa hapendwi lakini moyo wake uliamini kitu kimoja tu kwamba kuna siku angekuja kuwa na mwanaume huyo.
Aliendelea kusoma huku akiweka mipango yake ya muda mrefu, kwa kuwa alipokuwa akiingia mwaka wa tatu chuoni ndiyo kwanza Dickson alikuwa akianza mwaka wa kwanza jijini Dar, akaamua kutulia na kuisubiria siku ambayo aliamini kwamba mwanaume huyo angeukunjua moyo wake na kuwa naye tena.
Hakuacha kuwasiliana naye, alihakikisha anachati naye katika mitandao ya kijamii na hata kumpigia simu. Dickson hakumpenda Linda, alijitahidi kumnyamazia lakini msichana huyo hakukoma, bado imani yake ilimwambia kwamba kuna siku angekuwa na kijana huyo.
“Nimekukumbuka sana Dickson,” alisema Linda kwenye simu.
“Nashukuru sana!”
“Hivi bado unanipenda?”
“Nani? Mimi? Mbona umeniuliza hivyo?”
“Kwa kuwa nataka kujua!”
“Jamani! Sidhani kama unatakiwa kuniuliza hilo swali kwa kuwa ukweli unaujua!”
“Upi?”
“Linda! Hebu niambie, masomo yanasemaje huko?”

By Ahmad Mdowe 

ITAENDELEA………………………………………..

Where do you want to donate?

Traktir Kopi
Bank BCA - An. Asep Saepul Anwar/ Rek - 648xxxx
Treat the creator to coffee by giving a small donation. click the arrow icon above

Chapisha Maoni

Copyright ©BongoLife - All rights reserved.

Redesign by bloggun.xyz
Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
More Details