NAMTAKA MPENZ WANGU ARUDI SEHEMU YA 01

NAMTAKA MPENZ WANGU ARUDI

SEHEMU YA 1

WHATSAPP 0655585220

ZANZIBAR

“Unahitaji kuwa nani baadaye?” lilikuwa swali la kwanza mzee Jackson Gwamaka alimuuliza binti yake aliyeitwa Nandy aliyekuwa akisoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Kurasini, jijini Dar es Salaam.

“Nitataka kuwa muimbaji wa nyimbo za Injili, nitataka nimuimbie Mungu mpaka viwete watembee, vipofu waone na wenye matatizo mbalimbali waponywe,” alijibu binti huyo mrembo huku akimwangalia baba yake kwa sura iliyojaa tabasamu pana.

“Unahisi utaweza kumuimbia Mungu maisha yako yote?”

“Ndiyo! Nitamuimbia mpaka naingia kaburini. Nitataka nimtumikie yeye tu katika maisha yangu,” alijibu msichana huyo.

Mzee Gwamaka akamwangalia binti yake kwa mara nyingine, tabasamu pana likatawala usoni mwake. Alimpenda Nandy, alikuwa mtoto wake pekee katika maisha yake.

Moyo wake ulikuwa na faraja kubwa, alipenda kumuona Nandy akizungumzia kuhusu ukuu wa Mungu. Kila siku alimlea binti yake katika mazingira ya kidini huku akimwambia kuhusu ubaya wa wanaume.

Hakutaka kumuona binti yake akipotea, katika maisha yake alitamani kumuona akiendelea kumsifu Mungu mpaka pale atakapoingia kaburini. Mke wake, alifariki dunia siku alipokwenda kujifungua hospitalini. Moyo wake ulimuuma, alilia sana na ndiyo maana kwa Nandy alikuwa roho yake, faraja yake na hakutaka kumuona binti yake huyo akipotea.

Kila siku alimfundisha Nandy Neno la Mungu, alimwambia mambo mengi makuu ambayo Mungu alikuwa akiyatenda tangu kipindi cha Isaka,Yakobo na vizazi vingine vilivyofuata vikiwemo vya Mfalme Daudi na Suleimani.

Mbali na kutamani kumtumikia kumtumikia Mungu, Nandy alikuwa miongoni mwa mabinti waliokuwa na sura nzuri kupita kawaida japokuwa alikuwa akiishi kwenye umasikini mkubwa.

Mtaani hapo Kurasini alipokuwa akikaa, gumzo lilikuwa yeye tu. Alikuwa na umri mdogo lakini kila mtu aliyekuwa akimwangalia aliamini kwamba msichana huyo angekuja kutingisha sana siku za usoni.

Barabarani, wanaume walimtolea macho, kila aliyemwangalia hakuacha kumwangalia mara moja, alimwangalia mara mbili-mbili huku wengine wakidiriki kusimama na kumwangalia mpaka alipopotea katika macho yao.

Shuleni hakuwa msichana muongeaji, alikuwa mkimya huku muda mwingi akipenda kujisomea Kitabu Kitakatifu cha Biblia ambacho alikuwa akienda nacho mpaka shuleni.

Watu walimzoea kwa kumuita Sista kwani alionekana kupenda sana dini kuliko hata kusoma masomo ya darasani. Pamoja na sura yake nzuri, mvuto wake, Mungu alimbariki Nandy sauti.

Alijua kuimba, kila alipokuwa akisimama kanisani na kuongoza pambio watu walichanganyikiwa, sauti yake ilikuwa kali, iliyochujwa kiasi kwamba kila mmoja akamtabiria kuwa muimbaji mashuhuru nchini Tanzania miaka ya baadaye.

Siku zilikatika mpaka pale alipoingia darasa la saba na kumaliza. Uzuri wake uliongezeka, nyonga zikatanuka na kifua kuanza kuchuja. Urembo wake ukaongezeka na wanaume wakazidi kumpenda na hata wengine kuanza kumfuatilia kwa kuwa waliamini kwamba alikua hivyo alistahili kulala naye.

Wanaume wakaanza kumchombeza kwa maneno mbalimbali, wale wasiokuwa na aibu ya kutembea na watoto wadogo hawakumuacha, kwao, kitendo cha kifua kuonekana kimejaa tayari alionekana kuwa mkubwa.

Nandy aliogopa, hakukuwa na mwanaume aliyediriki kusimama naye, kila alipokuwa akiitwa, alikimbia, kwake, kwa malezi aliyokuwa amepewa na baba yake yalimfanya kuwaogopa wanaume kupita kawaida.

Wanaume hawakutaka kukata tamaa, kwao, hizo zilionekana kama changamoto na hivyo kuendelea kumfuatilia. Idadi ya wanaume waliokuwa wakimtaka ikaongezeka, kila mtu akatamani kulala na Nandy na kuwa mwanaume wa kwanza kufanya naye mapenzi katika maisha yake.

Nandy alijichunga, hata alipoingia kidato cha kwanza katika Shule ya Wasichana ya Jangwani bado msimamo wake ulikuwa uleule kwamba hakutaka kulala na mwanaume yeyote yule.

Kila walipokuwa wakitoka shuleni, wanafunzi wa Shule ya Wavulana ya Azania walikuwa wakisubiri nje, kila mmoja alitamani kumuona kwani alionekana kuwa msichana wa tofauti sana huku wengine wakihisi kwamba Mungu aliamua kumuumba msichana huyo wikiendi, kipindi ambacho alipumzika na kumuumba kwa udongo wa tofauti na wengine.

“Nandy!” alijikuta mwanafunzi mmoja akilitaja tu jina hilo.

“Amefanyaje tena?”

“We acha! Yule demu mkali bwana! Demu ni nuksi sana,” alisema mwanafunzi huyo huku akimwangalia rafiki yake na kuanza kucheka.

“Sasa wewe umegundua hilo leo?”

“Hapana! Nimegundua tangu siku ya kwanza nilipomuona. Ninasema hivyo kwa sababu amenichanganya sana. Nandy mzuri mno, demu bomba sana,” alisema mwanafunzi huyo.

Ni stori za uzuri wa Nandy ndizo zilizokuwa zimetawala midomoni mwa wavulana wengi. Walimpenda kwa kuwa alikuwa na sura nzuri, ngozi laini ambayo wanaume wengi iliwafanya kumfuatilia pasipo kumpata.

Nyumbani, mzee Gwamaka aliendelea kukandamiza misumali, kila siku ilikuwa ni kuongea na binti yake na kumwambia mambo mengi kuhusu wanaume, hakutaka kabisa kumuona binti yake akiingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa sababu tu hakutaka kuona akiumizwa.

Aliwaponda wanaume, akaufanya moyo wa Nandy kuwaona wanaume wana roho ya kinyama, aliwachukia na kila alipokuwa akiitwa, aliogopa na kukimbia.

Aliendelea na maisha hayo ya kuogopa wanaume mpaka alipofika kidato cha nne. Japokuwa alionekana kuwa mkubwa lakini bado aliendelea kuwaogopa wanaume kila siku, hakuacha kuwakimbia kila alipokuwa akiitwa na wanaume.

“Nandy! Tatizo nini kwani?” aliuliza mwanafunzi mmoja huku akiwa amemshika Nandy mkono, hakutaka kumuachia kwani aliwahi kumuita mara nyingi sana lakini msichana huyo alikuwa akimkimbia.

“Niachieee…”

“Nikuachie! Umenikimbia sana, leo niambie ukweli!”

“Ukweli wa nini Mike. Niachieeeee.”

“Nataka uniambie! Unanipenda au hunipendi?”

“Nimesema niachieeeee…”

“Nijibu kwanza.”

“Sikupendi! Sikutakiiiii…” alisema Nandy na kwa kutumia nguvu zake, akajitoa mkononi mwa Mike na kukimbia.

Hilo likaonekana kuwa tatizo, Nandy hakutaka kukubali, alipofika nyumbani tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumwambia baba yake kilichokuwa kimetokea.

Mzee Gwamaka alivimba kwa hasira, hakuamini kama kungetokea mvulana ambaye angemfanyia hivyo binti yake. Siku iliyofuata, ili kuonyesha kwamba binti yake hakutakiwa kuguswa akaelekea shuleni huko na kuwaambia walimu ambapo baada ya Nandy kuulizwa akamtaja kijana huyo.

Adhabu iliyotolewa siku hiyo, hakukuwa na mwanafunzi aliyediriki kumsogelea Nandy na kumwambia kitu chochote kuhusu mapenzi, wote walimuogopa kwani kila walipokumbuka mzee Gwamaka jinsi alivyokwenda shuleni hapo akiwa amevimba kwa hasira, hakukuwa na mtu aliyediriki kumsogelea.

Mpaka Nandy anamaliza kidato cha nne shuleni hapo bado hakuwa amemjua mwanaume yeyote yule. Aliendelea kujitunza kujitunza huku akimwambia baba yake kwamba malengo yake katika maisha yake yalikuwa ni kumtumikia Mungu mpaka anaingia ndani ya kaburi.

Baada ya kukaa nbaada ya kumaliza kidato cha nne ndipo walipotangaziwa kanisani kwao kwamba kungekuwa na mkutano mkubwa wa injili ambao ulitarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Jangwani huku mhubiri mkubwa wa Kimataifa, Benn Hinn akitarajiwa kuhubiri katika viwanja hivyo.

Hiyo ilikuwa ni taarifa njema, kwa kuwa alikuwa na sauti nzuri huku akipewa uongozi katika kuimba pambio, Nandy akaambiwa ajiandae kwani alitakiwa kuongoza pambio katika kipindi chote cha mkutano huo.

Kwake, nafasi hiyo ilikuwa kubwa mno. Alimfahamu muhubiri huyo wa kimataifa aliyekuwa akizunguka dunia nzima huku akilihubiri Neno la Mungu, kitendo cha kuteuliwa kuongoza kikundi cha pambi katika mkutano huo ilionekana kama ndoto yake kuwa kweli.


By Ahmad Mdowe 


ITAENDELEA……………………..

Where do you want to donate?

Traktir Kopi
Bank BCA - An. Asep Saepul Anwar/ Rek - 648xxxx
Treat the creator to coffee by giving a small donation. click the arrow icon above

Chapisha Maoni

Copyright ©BongoLife - All rights reserved.

Redesign by bloggun.xyz
Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
More Details