SALA YA SARAH SEHEMU YA KWANZA (01)

RIWAYA : SALA YA SARAH.

MTUNZI : ALEX KILEO.

0766 404 747

SEHEMU YA KWANZA.


UTANGULIZI.


Katika maisha tunapitia nyakati tofauti na ngumu sana, ila katika maisha yetu ya kawaida yupo wengi ambao tunaangaika kwa ajili ya kupata ridhiki tu, tunaamini katika utafutaji ili tujiepushe na njaa na matatizo mengine ambayo utatuka kwa pesa.


Pia kuna watu ambao hawajajenga ila uishi, hawajalima wala kutafuta ila wanakula, asilimia kubwa ya watu hawa uwa wamezikuta mali zilizotafutwa na babu zao au baba zao na wao hurithishwa bila kuvuja jasho, mara nyingi vitu vya mirathi uwa na migogoro, nakuapia msomaji wangu, hakuna kitu cha mirathi kisicho na migogoro hususani kikiachwa kwa mtu zaidi ya mmoja.


Riwaya yetu itagusa sana upande huo ila ndani kutakuwa na matukio yatayokuacha na taharuki za hatari, kama kawaida yangu napenda sana kusimulia vitu vya kipelelezi na mapigano ndani yake, yote yamo humu.


Riwaya hii ni kitu tu cha kubuni na wala sio simulizi ya kweli na wala haikuwahi kuandikwa sehemu yoyote ile duniani, kama itatokea kufanana na hadithi yoyote ile, basi ujue ni mawazo ya waandishi tu yamegongana na kamwe haiwezi kufanana hadithi yote.


Nawakaribisha tena washkaji wangu ili tulisongeshe dude.


----------------------

MWANZO. 

-----------------------


Ni nyakati za alasiri jua likiwa bado halijapoa ukali wake na baadhi ya watu wakiwa katika pilika pilika za kujitafutia riziki zao kwa ajili ya kuendesha maisha yao katikati ya jiji.


Ndani ya hoteli moja kubwa na maarufu hapa mjini kulikuwa na kikao kidogo kinaendelea kati ya watu wawili, mwanaume mmoja na mwanamke mmoja, hawa watu ni ndugu, mtu na Dada yake, yaani mtoto wa mkubwa na mtoto wa mdogo.


Mwanaume anaitwa Denis Michael Dege alimaarufu alikuwa anaitwa Taita, na mwanamke anaitwa Mage Stewart Dege, ndani ya kikao kuna kitu kilikuwa kinajadiliwa, walikuwa wanajadili mirathi ambayo iliachwa na baba zao ambao walikuwa ni ndugu wa baba na mama mmoja, baba zao walishafariki na wakaacha mali nyingi ambazo walizirithi kutoka kwa baba yao.


Bahati nzuri asilimia kubwa ya mali walikuwa wameshagawana, walichokuwa wanajadili ni nyumba mbili tu ambazo zilikuwa katikati ya mji.


"Nimeshapata Mteja wa nyumba moja ile ya ghorofa" Taita aliongea kisha akagida maji yaliyokuwa katika glass,


"Anatoa shilingi ngapi?" Magreth aliuliza huku akimuangalia usoni Taita,


"Bilioni moja" Taita alijibu,


"Hapana, hiyo haitoshi, kwa sehemu ilipo ile nyumba ni bilioni mbili, nilifuatilia wizara ya ardhi na makazi na bei niliyoambiwa ni hiyo, hata wewe unajua hilo" Magreth aliongea huku akiendelea kumuangalia kaka yake huyo,


"Nilijua tu ni lazima ulete kikwazo, kwani kuna ubaya gani tukiuza hiyo nyumba bilioni moja? kwani uliijenga wewe?" Taita aliuliza kwa hasira


"Unadhani aliyeijenga angekubali kuuza kwa bei hiyo?" Magreth aliuliza huku sura yake ikiwa imejaa ujeuri,


"Kwanza unatakiwa kujua wewe ni mwanamke tu, hata tulivyogawana mali za hawali nilifanya ubinadamu tu, kihalisia wewe hutakiwi kupata kitu, mimi ndio mrithi wa mali zote" Taita aliongea na kutoa cheko la dharau,


"Mpuuzi wewe usilete mambo ya kizamani, dunia ya leo ni haki tu kwa wote" Magreth aliongea kwa hasira,


"Ebu acha ukorofi Mage, ujue Nina shida na hela?" Taita aliongea huku akitabasamu,


"Una shida gani wewe, kila kitu unacho, una majumba una hela na una vitega uchumi vya kila aina" Magreth aliongea kwa kufoka,


"Basi toa uamuzi, nyumba iuzwe au isiuzwe kwa bei hiyo?" Taita aliuliza,


"Nyumba haiuzwi kwa bei hiyo" Magreth alijibu,


"Alafu yule mume wako ndiyo anaekushauri ujinga, yaani mkikaa hamna cha maana mnachojadili zaidi ya hizi mali, tafuteni za kwenu" Taita aliongea kwa dharau, uwa hakasirikagi huyu bwana mwenye umri wa miaka thelathini na mbili, uwa anatabasamu muda wote.


"Hatujaja kuongelea familia yangu hapa, tukisema tuongelee familia basi tuanze na wewe usiye na mtoto na bado una mke na mmeoana miaka saba iliyopita" Magreth aliongea kwa hasira,


"Nadhani tumemaliza, nyumba nitaiuza kwa hiyo pesa na nitakuletea milioni mia tano, kama utazikataa nitazichukua zote" Taita aliongea na kunywa maji tena,


"Sheria zipo" Magreth aliongea kwa hasira,


"Mwisho wa majadiliano, hati zote ninazo mimi" Taita aliongea na kunyanyuka kisha akaanza kuondoka na kumuacha Dada ake akimuangalia tu mpaka alipotoka kwenye ule mlango wa hoteli ambao ulikuwa wa vioo, Taita alitoka na kuingia kwenye gari la kifahari na kuondoka zake.


Magreth aliendelea kukaa kwa muda pale hotelini huku akionekana mwenye hasira, Dada huyu ana miaka ishirini na nane tu.


Baada ya kukaa kwa muda alinyanyuka na kutoka nje ya ile hoteli na kuingia kwenye gari lake dogo la kawaida na kuondoka zake kurudi nyumbani kwake.


Magreth ni mfanyakazi wa serikali katika wizara ya madini, ana cheo cha juu kiasi, ameolewa na ana watoto wawili, wa kwanza ni wa kike anaitwa Sarah, ana miaka mitano na wa pili anaitwa Sebastian, ana miaka mitatu tu.


Magreth alirudi kwake na kuingia mpaka sebuleni, akalakiwa na mwanaye mkubwa aitwae Sarah na kumkumbatia mama yake kisha akamsalimia,


"Shuleni leo mmefundishwa nini mwanangu?" Magreth alimuuliza Sarah,


"Kusoma na kuandika" Sarah alijibu,


"Hakuna homework leo?" Magreth alimuuliza mwanae,


"Ipo" Sarah alijibu,


"Umeshakula?" Magreth aliuliza,


"Tayari mama, nimeshiba" Sarah alijibu,


"Haya, nenda mezani ukafanye homework yako" Magreth aliongea kisha akaenda moja kwa moja kwenye kochi na kumbusu mume wake aliyekuwa amekaa hapo juu ya kochi, huyu bwana anaitwa Isack Senga, ni mlemavu wa miguu, hana miguu yote miwili, ilikatwa baada ya kupata ajali ya gari.


Magreth alimfikia mume wake na kumbusu kwenye paji la uso,


"Taita anasemaje?" Isack aliuliza,


"Anataka kuuza ile nyumba ya ghorofa kwa lazima" Magreth alijibu huku akikaa kwenye kochi,


"Sio habari mbaya, anataka kuuza shilingi ngapi?" Isack aliuliza,


"Bilioni moja, aisee hiyo bei ni ya nyumba za kawaida katika eneo lile, na sio za ghorofa" Magreth alijibu,


"Kwa hiyo bei inakuwa sio sawa. Muafaka gani mmefikia?" Isack aliuliza,


"Hakuna muafaka, alichoamua ni kuuza kwa nguvu, kesho nitaongea na mwanasheria wangu" Magreth aliongea,


"Fanya hivyo, maana yule ndugu yako hana nia nzuri" Isack aliongea,


"Umeshakula mume wangu?" Magreth alimuuliza mumewe,


"Hapana, nilikuwa nakusubiri" Isack alijibu,


"Ngoja nikaoge basi" Magreth aliongea na kunyanyuka akaelekea chumbani na kumuacha mume wake akimuangalia huku akitabasamu.


Ndivyo ilivyo nyumba hii, upendo umetawala kila kona, utafikiri wameoana juzi au jana.


Baada ya saa nzima Magreth alitoka chumbani huku akiwa ameshaoga na amevaa nguo za nyumbani. Akaelekea moja kwa moja jikoni na kuchukua chakula ambacho kilikuwa kimeshaandaliwa na msichana na kazi, akakipeleka mezani na kuanza kula na mume wake huku wakiongea mawili matatu ya kifamilia.


___________

USIKU

____________


Yapata kama mida ya saa nne na nusu usiku, watoto na Dada wa kazi wakiwa tayari wamekwishalala, Magreth na Isack walikuwa wapo sebuleni wakiangalia runinga, kipindi cha dini, wakiwa wamekolea kwenye imani walisikia mlango wa mbele wa nyumba yao ukigongwa, haikuwa ajabu kwao kugongewa mlango muda huo, maana hiyo hali walishaizoea kutokana na misaada wanayotoaga kwa majirani zao, kwa hiyo usiku kama huo kupokea ugeni ukiitaji msaada ni kawaida.


Magreth akasimama na kwenda moja kwa moja kufungua mlango, alipotoa kichwa nje alikutana na mdomo wa bastola iliyokuwa imeshikwa na kijana mweupe aliyekuwa amejichora tatoo karibu mwili wake wote,


"Bila kelele wala usumbufu rudi ndani" Kijana aliongea na kumfanya Magreth ageuke taratibu na kurudi ndani na yule kijana akaingia huku bastola ikiwa mkononi, Isack alipoona hivyo nae akashtuka, hakuwa na cha kufanya maana hakuwa na miguu.


"Vipi unataka kukimbia? Kimbia mi sitokupiga risasi" Kijena mwenye tatoo aliongea kwa dhihaka huku akitabasamu, kisha akaikagua ile nyumba kwa macho kuyazungusha sebule nzima, alipolizika akapiga mluzi kwa nguvu na kufanya Magreth na Isack waendelee kushangaa bila kujua lengo la yule kijana.


Sekunde kadhaa tu baada ya ule mluzi, walishangaa kuona sebule ikivamiwa na vijana kama kumi na nyuma yao alikuwepo Taita huku akiwa ameshika makabrasha na sigara yake kubwa mdomoni na pia aliongozana na kijana mwingine nadhifu aliyevaa suti nyeusi,


"Dada mage, ni vizuri nimewakuta wote wawili maana mtatoa jibu sahihi" Taita aliongea na kujiweka kwenye kochi,


"Wewe shetani unadiriki kuniteka ndani ya nyumba yangu?" Magreth aliongea kwa uchungu huku akimuangalia Taita,


"Sijaja kujadili utekaji, nimekuja na mwanasheria wangu huyu hapa, nahitaji upige sahihi ili kuidhinisha nyumba kuuzwa" Taita aliongea huku akimuangalia yule kijana nadhifu waliyeingia nae,


"Ndio upuuzi uliokuleta huo? usitegee nitafanya hivyo" Margret aliongea kwa hasira,


"Kama ni suala la nyumba, ngoja kesho kukuche ili dada yako nae aje na mwanasheria wake ili mfikie makubaliano" Isack aliongea na Taita akamuangalia kwa jicho Kali, kisha akampa ishara yule kijana mwenye tatoo na yule kijana akakafyatua risasi iliyomkuta Isack mkono wa kushoto begani na kufanya atoe ukelele na Magreth akamkumbatia,


"Shiiiiiii hupaswi kuingilia kesi ya mali zangu na dada yangu, unatakiwa ukae kimya, nitakuondoa na mikono yako ubaki na kiwili wili tu" Taita aliongea huku akimuangalia Isack aliyekuwa Analia kwa uchungu,


"Jamani fanyeni haya, ila sitaki wanangu ndani wajue kinachoendelea" Isack aliongea huku akilia,


"Kumbe na watoto wapo?, Trigger kawalete wajomba zangu" Taita aliongea kisha yule Jamaa mwenye tatoo akaelekea vyumbani na kuanza kuwatafuta watoto, baada ya muda alirudi na watoto wawili na dada wa kazi,


"Shikamoo anko" Sarah alimuamkia Taita, masikini hakujua hata kinachoendelea,


"Marhaba, njoo anko" Taita alijibu huku akitabasamu na kumpakata Sarah na mdogo wake,


"Magreth saini wanachotaka, cha muhimu watoto wetu wabaki Salama" Isack alimwambia mkewe ambaye hakupinga, aliomba makabrasha na kusaini panapotakiwa,


"Safi sana" Taita aliongea huku akipiga makofi,


"Kinachofuata" Trigger aliuliza huku akimuangalia Taita,


"Funga kamba hao mbwa" Taita aliongea huku akisimama na alikuwa amewabeba Sarah na mdogo wake,


"Si tayari nimefanya utakacho? Kamba nifungwe za nini sasa?" Magret aliuliza lakini hakujibiwa, vijana walimfunga kamba yeye, mume wake na msichana wa kazi, kisha wakawatia vitambaa mdomoni ili wasipige kelele.


Taita akatoka nje akiwa na watoto,


"Tunafanyaje boss?"Trigger akiuliza, trigger ni yule kijana mwenye tatoo,


"Choma moto nyumba, wanatakiwa wafe" Taita aliongea huku akielekea kwenye gari na watoto,


"Tajiri eeh, huyu mtoto wa kike ni mkubwa, ana akili na anajua kinachoendelea, nae hatakiwi kuishi" Wakili alimshauri Taita,


"Kweli kabisa, kwanza atakuja kuwa msumbufu kama mama yake" Taita aliongea kisha akafungua mlango wa gari na kumtupa chini Sarah, Sarah akaanza kulia,


"Kitanzi, huyu nae kamtupe ndani, achomwe moto" Taita aliongea na kisha kijana wake mmoja aitwae kitanzi akambeba na kwenda kumtupa Sarah ndani, kisha milango yote ikafungwa kwa nje, nyumba ikamwagiwa mafuta na kuwashwa moto, nyumba yote ikashika moto,


"Tupotee" Taita alimwambia dereva wake na kisha gari ikaanza kuondoka taratibu na magari mengine waliyokuja nayo yakafuata...............


**********ITAENDELEA***********

Where do you want to donate?

Traktir Kopi
Bank BCA - An. Asep Saepul Anwar/ Rek - 648xxxx
Treat the creator to coffee by giving a small donation. click the arrow icon above

Chapisha Maoni

Copyright ©BongoLife - All rights reserved.

Redesign by bloggun.xyz
Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
More Details