FAHAMU KUHUSU OPERATION ENTEBE | OPERATION THUNDERBOLT

Operation hii maarufu ya kijeshi iliandaliwa kwa kipindi cha siku saba na ikafanyika kwa muda wa dakika tisini tu! baada ya ndege ya shirika la anga la Ufaransa ilitekwa


OPERATION ENTEBE

Movie ilianza tarehe 27 mwezi wa saba mwaka 1976 ambapo ndege ya shirika la anga la Ufaransa ilitekwa.
Ndege hiyo ilikuwa inafanya safari zake baina ya Tel-Aviv nchini Israel na kwenda kutua uwanja wa ndege wa Charles De Gaulle mjini Paris nchini Ufaransa ikipitia Athens nchini Ugiriki.

On that fateful day,ndege iliondoka mjini Tel-Aviv ikiwa na jumla ya abiria 256 ambapo ilipofika Athens wapo walioshuka na kuruhusu kuingia abiria wengine 58 na safari ya kuelekea Paris ikaendelea.
Miongoni mwa abiria waliopanda pale Athens walikuwepo vijana wanne ambao waliiteka ndege hiyo mara tu baada ya kuruka Athens na kumuamuru rubani aelekee Benghazi nchini Libya.
Walipofika Benghazi waliijaza mafuta ndege na waliwaruhusu abiria kupunga upepo na baada ya masaa saba waliamuru ndege ielekee Entebe nchini Uganda.

Walipofika Entebe, abiria wote na wahudumu wa ndege waliswekwa kwenye jumba la airport ya zamani na hapo pia watekaji wengine wanne waliongezeka na idadi yao ikawa jumla wanane.

Kesho yake tarehe 28 kundi la Popular Front For Liberation Of Palestine(PFLP) lilitangaza kwamba wao ndio wameiteka hiyo ndege na walikuwa na masharti makuu mawili tu ili wawaachie salama abiria waliokua kwenye ndege hiyo(Idadi yao kubwa walikuwa ni wayahudi au raia wa Israel).
Sharti namba moja lilikuwa ni serikali ya Israel ikubali kuwaachia huru wafungwa wa Kipalestina zaidi ya 40 inayowashikilia kwenye magereza yake nchini Israel na pia wengine 12 wanaoshikiliwa na serikali nyingine duniani kote.
Pili,walitaka walipwe kiasi cha fedha $5million(dola za kimarekani milioni tano)

Baada ya tukio kutangazwa sana kwenye vyombo vya habari watu walitarajia kusikia neno kutoka kwa serikali yoyote(hasa Israel na Ufaransa) lakini cha ajabu ikawa kimya!

HALI ILIVYOKUWA NCHINI ISRAEL


Shirika la kijasusi la Israel,MOSSAD lilikuwa la kwanza kupata taarifa za kutekwa kwa ndege hiyo na likawasilina na wakuu wa nchi kuhusu hali halisi na kukaibuka hali ya sintofahamu kubwa sana miongoni mwa viongozi wa juu wa Israel.
Walikuwa na uhakika kwamba ndani ya ile ndege zaidi ya abiria 100 walikuwa ni wayahudi kwahiyo wao ndio walikuwa wenye 'msiba' na target ya watekaji kwa vyovyote ingekuwa ni hao mateka wa kiyahudi tu.
Baraza la mawaziri likiongozwa na waziri mkuu Yitzahak Rabin lilikutana usiku huohuo kwa dharula na kuanza kujaribu kupata namna ya kuokoa raia wao.
Ikumbukwe kwamba kwa miaka yote serikali ya Israel imekuwa ikishikilia sera yake ya kutokukuwa tayari kukaa meza moja ya majadiliano na vikundi vyote vya kiarabu vinavyoipinga kwa hiyo hili pia lilivutia watu wengi duniani kuona kama watakubali kuwapoteza raia wao namna ile kisa tu hawataki majadiliano na waarabu.
Maana kukubali yale masharti ilikuwa haiwezekani kama hakutakuwa na majadiliano!
Hapo ikawa mtihani mkubwa sana kwa mawaziri wa Israel.
Katika kikao hicho kulitokea kutokukubaliana kimaoni baina ya waziri mkuu na waziri wa ulinzi bwana Shimon Peres ambapo waziri mkuu alikuwa tayari kukubali masharti ya watekaji na aliungwa mkono na kundi kubwa la mawaziri ila waziri wa ulinzi alikuwa kinyume na wazo hili.
Yeye aliwaambia wampe siku kadhaa aweze kusuka mpango wa kuwakomboa mateka kijeshi maana aliamini kabisa deadline iliyowekwa na watekaji ya tarehe 1 July ni siku nyingi mno.
Mawaziri wengi walimpinga wakamwambia kwamba yeye anasema hivyo kwasababu sio mwanasiasa wa kupigiwa kura na wananchi kwahiyo mateka watakapouawa hatoathirika chochote..
Siku tatu mfululizo Peres alikuwa anajaribu kuwashawishi mawaziri wakubali na wapitishe mpango wa kijeshi.

Wakati huohuo,
Mossad na IDF(Israel Defense Forces) hawakuwa wamelala.
Walikesha usiku kucha kujaribu kuweka mezani mipango ya uvamizi na taarifa za uwanja wa ndege wa Entebe ili kama ikiamriwa kuivamia Entebe wawe tayari.

KOSA KUBWA KWA WATEKAJI!?


Ni ukweli usiopingika wala kuwa na shaka yoyote kwamba kilichowaponza watekaji ni huruma yao!
Kosa la kwanza lilianzia walipofika uwanja wa ndege wa Benghazi ambapo walimuonea huruma mwanamke mmoja wa kiingereza aliyekuwa na mimba kubwa alipoanza kulia kwamba anahisi amepata 'miscarriage' wakamruhusu aondoke!
Yule mwanamke baadae alisema kwamba aliwadanganya tu.
Na alipofika London watu wa kwanza kumpokea walikuwa ni maafisa wa Mossad na walimuhoji akawapa taarifa muhimu.

Kosa lingine,
Walipofika Entebe,
Wakaona ni bora wawachie mateka kutoka mataifa mengine tofauti na Israel zaidi ya 130 hivyo wakabaki na wayahudi tu wapatao 94 pamoja na wahudumu wa ndege hiyo wapatao 12.
Pia kati ya mateka waliowaachia walishindwa kumtambua jamaa mmoja ambaye ni askari wa IDF aliyekuwa na uraia wa nchi mbili hivyo aliwapa passport yake ya Uingereza na wakajua ni muingereza(this was a grave mistake)

Mateka waliochiwa walihojiwa kwa kina na hakika walitoa taarifa muhimu sana.
Yule askari aliweza kutoa kila taarifa muhimu ikiwemo namna ambavyo watekaji ni waoga na hawana uzoefu pia alitoa namna maaskari wa Uganda wanavyoilinda hiyo airport na madhaifu aliyoyaona.Hatimaye wakuu wa Mossad na IDF wakaenda kwenye vikao vya baraza la mawaziri kuwahakikishia kwamba wanauhakika wa kufanya mission ya uokozi yenye mafanikio ikiwa wataruhusiwa na kupewa ushirikiano.
Mawaziri wengi wakakubali ila waziri mkuu akawa bado anaogopa sana.

TURUDI KWENYE VIKAO VYA BARAZA LA MAWAZIRI.


Ukizingatia kwamba taarifa ya watekaji ilidai kwamba mwisho wa kufanya maongezi ni tarehe moja mwezi wa saba vinginevyo wayahudi wote walioshikiliwa wangeuawa palepale Entebe!
Muda ulikuwa unaenda kwa kasi huku waheshimiwa wakiwa wanashindwa kupata muafaka wa pamoja kama serikali.
Kwanza waliamua kuanza kumshawishi raisi wa Uganda aache kuwaunga mkono watekaji. Wakafanya mawasiliano na Iddi Àmin ambaye ndio alikuwa amewapa hifadhi watekaji kwenye ardhi ya nchi yake.
Walimpa kazi hiyo swahiba wake afisa mstaafu wa jeshi la Israel(IDF) bwana Baruch Burkah ambaye anajuana na Amin kama marafiki kwani waliwahi kuwa pamoja nchini Uganda wakati Idd Amin akiwa jenerali wa majeshi ya Uganda na yeye akiwa mkuu wa kikosi maalumu cha Israel kilichokuwa kinatoa mafunzo ya kijeshi kwa maaskari wa Uganda.
Amini akamkatalia swahiba wake na akamwambia hawezi kuwasaliti PFLP.
Iliposhindikana ikabidi waombe msaada Washington kwa raisi Jimmy Carter awasaidie kumshinikiza Anwar Al Saadat wa raisi wa Misri aongee na Idd Amin na viongozi wa PFLP wawaachie mateka wao.
Hii pia ikafeli! Kwani Saadat alikataa.
Kwahiyo wakawa na zilezile njia mbili tu!
Aidha wavamie Entebe au wakubali masharti ya watekaji!

Masaa machache kabla ya muda wa deadline kuwadia hatimaye walikubali kuivamia kijeshi Entebe ila wakawa na uhaba wa muda!
Kukosekana kwa muda wa kutosha wa kufanya maandilizi kuliwalazimu wavunje ile sera yao thabiti ya kujadiliana na waarabu!

Waziri mkuu akajitokeza hadharani kuitangazia dunia kwamba 'baraza la mawaziri la taifa la Israel limekubaliana kwa pamoja kukaa meza moja na PFLP na kwamba wapo tayari kutimiza masharti yote waliyopewa maana uhai wa raia wa Israel ndio kipaumbele namba moja kama serikali'
Lakini tu aliwaomba watekaji waongeze muda kidogo ili wakamilishe taratibu zote.

WATEKAJI WANAFANYA KOSA LINGINE HAPA!
Baada ya majadiliano ya muda mrefu baina ya PFLP,Amin na Israel hatimaye PFLP wakakubali ombi la serikali ya Israel la kusogeza mbele muda wa mwisho 'deadline' mpaka tarehe 4 July.(This was the graviest mistake)

MIPANGO YA UVAMIZI


MOSSAD na IDF walikuwa wameshakusanya taarifa zote za kiintelijensia kuhusu ambazo zingewawezesha kuingia Entebe na kurudi Israel salama wakiwa na mateka wao.
Siku zote hizo walikuwa wakiwahoji mateka walioachiliwa na wakawa wanakusanya taarifa kwa kina na kwa usahihi wa hali ya juu.
Baadae wakagundua kwamba kampuni iliyojenga majengo ya zamani ya airport ya Entebe ambapo ndio mateka wamehifadhiwa ni kampuni ya kiisrael!
Kwahiyo kazi ya kudesign mpango wa uvamizi ikawa rahisi sana!

Mpango wa kwanza ulipendekezwa kwamba watumwe makomando kuivamia Entebe kupitia maji ya ziwa victoria ambapo uwanja wa ndege wa Entebe upo pembezoni mwa ziwa hilo.
Hii ilishindikana mara baada ya kupata taarifa kwamba upande ule wa Entebe huwa una mamba wengi sana kutoka mto Nile hivyo isingekuwa salama hata kidogo kwa makomando wao.

Ndipo ukaletwa mpango uliokubalika na maafisa wengi wa kuivamia Entebe kupitia ardhi na anga.
Mpango huu ukawa mgumu pia kwani ili ufanikiwe walihitaji kuungwa mkono na moja kati ya nchi za Afrika Mashariki.
Waliichagua Kenya ambapo kulikuwa na mtaji mkubwa tu wa matajiri wa kiyahudi ambapo matajiri hao wakamshawishi raisi Jomo Kenyatta aruhusu ndege za IDF zitue kwenye uwanja wa ndege wa pale Nairobi(JKIA) naye bila hiyana akakubali!

Kwa taarifa walizokuwa nazo ni kwamba rais Amin alikuwa anaenda pale uwanja wa ndege kusalimiana na mateka kila siku kwahiyo wakaandaa magari ya msafara wa kama ule wa rais Amin na sare za kijeshi za Uganda.
Kikaandaliwa kikosi kazi cha makomando 100 kwenda kufanya mision ya uokoaji Entebe!

Masaa machache kabla ya deadline usiku wa tarehe 03 kuamkia hiyo tarehe 04 kwa majira ya Entebe ndege kubwa nne za kijeshi za IDF zilikuwa zinaruka juu kidogo ya bahari ya Sham mita kama 30 tu hivi ili kuzuia kunaswa na radar za Misri,Sudan au Saudi Arabia.
Walipokaribia kuimaliza bahari ndege zikakata kona kuelekea kaskazini upande wa kusini mwa Djibout na wakatembea mpaka maeneo ya Somalia na wakaunga kwa Magharibi mpaka ukanda wa bonde la ufa la Kenya.
Ndege mbili zikanyoosha mpaka Nairobi na zingine mbili zikanyooka moja kwa moja Entebe.

Unashangaa?
Hiyo OPERATION THUNDERBOLT ndio ilikuwa ipo kwenye utekelezaji hapo!

Zile ndege mbili zikafika Entebe na harakaharaka huku moja ikifungwa kifaa cha kuharibu kwa muda rada ya pele Entebe Airport.
Muda mfupi baadaye magari yanayoashiria msafara wa rais Amin yakateremka na kuanza kuongoza ulipo uwanja wa ndege wa zamani!
Maaskari wa jeshi la Uganda waliokuwa wanaulinda ule uwanja wakadhani ni rais anakuja kusalimia mateka.
Ila kuna maafisa walikuwepo pale muda ule na walikuwa wanafahamu kwamba rais Amin amebadilisha magari yake siku mbili zilizopita!
Wakaamuru ule msafara usimame!
Waaisrael wasikie tu,wakaona wale maafisa wanakuwa kizuizi ikaamuliwa wapigwe risasi kwa pisto zenye viwambo vya sauti.
Bahati mbaya sana mmoja hakufa!
Akapiga kelele!
Ikaibuka vita sasa!
Lengo la wale makomando kwa mujibu wa operation ile lilikuwa ni kutokumdhuru askari yoyote wa jeshi la Uganda kama hakutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
Ila kwa hali ile ikabidi wavunje hiyo taratibu na kuanza kuwashambulia!
Ndani ya dakika pungufu ya 30 maaskari wote 40 wa jeshi la Uganda wakawa wamelala chini kwa kufa na jamaa wakasogea mbele walipo mateka na watekaji.
Muda huo huo, ndege mbili zilizopitia Nairobi zikaanza kutua pale na kuharibu defesnse system yote ya uwanja.

Makomando walipolisogea jengo ambalo meteka walikuwa wamehifadhiwa wakatangaza kwa lugha ya Kiebrania kwa kutumia kipaza sauti kwamba "Kila mtu alale chini tunafyatua risasi sisi ni IDF" wale mateka wote wakalala chini na wale watekaji wakaanza kurusha risasi kuelekea kwa makomando wa Kiisrael.
Baada ya majibizano ya muda wa dakika kama hamsini hivi hatimaye wale watekaji wote wakawa wameuawa na wao wakawa wameua mateka watatu tu.

Wakati kila kitu kinaonekana kuisha na mateka wanapakiwa kwenye ndege kuna askari mmoja wa jeshi la Uganda hakufa!
Alikuwa anajifanya kalala chini amekufa kumbe mzima! Akamuangalia mkuu wa kikosi amekaa wapi akamfyatulia risasi kadhaa na akafanikiwa kumuua!
Aliyekufa ni mkuu wa operation aliyekuwa anaitwa Yonathan Netanyahu ambaye ni kaka wa Benjamin Netanyahu,waziri mkuu wa sasa wa Israel!

Huo ndio ukawa mwisho wa 'Operation Entebe' au kwa code name ya kijeshi waliipa jina la OPERATION THUNDERBOLT.

Operation hii maarufu ya kijeshi iliandaliwa kwa kipindi cha siku saba na ikafanyika kwa muda wa dakika tisini tu!

Where do you want to donate?

Traktir Kopi
Bank BCA - An. Asep Saepul Anwar/ Rek - 648xxxx
Treat the creator to coffee by giving a small donation. click the arrow icon above

Chapisha Maoni

Copyright ©BongoLife - All rights reserved.

Redesign by bloggun.xyz
Cookie Consent
We serve cookies on this site to analyze traffic, remember your preferences, and optimize your experience.
More Details